May 07, 2024 06:38 UTC
  • UNRWA: Hatutaondoka Rafah hata kwa maafa yatakayosababishwa na uvamizi wa Israel

Huku kukiwa na ripoti kwamba Wapalestina 100,00 wameamriwa kuhama Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza kabla ya uvamizi wa kijeshi uliopangwa kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa huduma za kibinadamu yamesisitiza kuwa hayana nia ya kuondoka katika mji huo muhimu zaidi kwa mahitaji ya misaada ya kibinadamu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA limeeleza kwamba halitaondoka Rafah, bali litaendelea kuweko katika eneo hilo kwa kadiri inavyowezekana na litaendelea kusambaza misaada ya kiutu ya kuokoa maisha ya watu.

Katika ujumbe lilioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X, UNRWA limesema: “shambulio la Israel dhidi ya Rafah litamaanisha kuwa raia zaidi watapata machungu na kufa na madhara yake yatakuwa makubwa na ya kutisha kwa watu milioni 1.4 walioko kwenye eneo hilo”.

Kauli ya janga linaloweza kutokea Rafah imetiliwa mkazo pia na Shirika la  Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF ambalo limeonya kuwa kuzingirwa kijeshi Rafah sambamba na kufanywa operesheni za ardhini za kijeshi kutasababisha janga kubwa kwa watoto 600,000 waliopewa hifadhi kwenye eneo hilo. 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa mjini New York imekumbusha kuwa amri ya kuhamia Rafah kusini mwa Ghaza iliyotolewa mwezi Oktoba mwaka jana na utawala wenyewe wa Kizayuni wa Israel imelifanya eneo hilo sasa kuhifadhi watu wapatao milioi 1.2, nusu yao wakiwa ni watoto ambao wanaishi kwenye mahema au nyumba zisizo kamilifu.

Sambamba na mamlaka za utawala ghasibu wa Israel kutoa vitisho vya kufanya mashambulizi ya ardhini dhidi ya mji wa Rafah, jana Jumatatu jeshi la Kizayuni lilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuwahamisha wakazi wa eneo la mashariki mwa mji huo na kuwapeleka mji wa Khan Yunis.../