May 08, 2024 07:04 UTC
  • Baada ya mafuriko, tishio la kipindupindu lavikabili vitongoji duni Nairobi, Kenya

Mvua kubwa na mafuriko vinaendelea kushuhudiwa nchini Kenya ambapo hadi sasa vimesababisha watu 228 kufariki dunia.

Wikiendi hii, mamlaka husika nchini Kenyya ziliwahamisha raia, wakati mwingine kwa nguvu, wanaoishi katika maeneo ya mafuriko. Hii ilikuwa hasa katika vitongoji duni vya Nairobi. Lakini watu hawa wanakabiliana na shida nyingine kama kuenea kwa magonjwa. Ripoti kutoka Kibera, makazi duni makubwa zaidi katika mji mkuu.

Mashirika mbalimbai yametoa onyo kuhusiana na uwezekano wa kutokea mlipuko wa magonjwa hasa kipindupindu hasa katika maeneo yenye huduma duni za kijamii kama maji.

Kwa mujibu wa Dk Dalmas Otieno, tuna wasiwasi wa kutokea kwa mlipuko wa janga la kipindupindu: "Vitongoji duni vyote viko hatarini, kwa sababu maji machafu huvamia maeneo yote ambayo mifereji ya maji ni duni. Mlipuko wa Kipindupindu unaweza kuwa hatari sana hapa. Kwa hiyo moja ya mambo tunayojaribu kufanya ni kuwafundisha watu jinsi ya kushughulikia usafi wa maji na kushughulikia magonjwa ya kuhara mapema. "

 

Kaunti zilizoathiriwa zaidi kwa mafuriko huko Kenya ni pamoja na  Homa Bay, Kajiado, Nakuru, Mandera na Nairobi ambapo zinaendelea kukabiliana na mafuriko makubwa ambayo yamesababisha usumbufu mkubwa kwa maisha ya kila siku na shughuli za kiuchumi.

Inaelezwa kuwa, maelfu ya wakimbizi katika nchi za Afrika Mashariki wamelazimika kuhama maeneo waliyokuwa wamepata hifadhi kufuatia  mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko yaliyoambatana na maafa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) limetaja wakimbizi walioathiriwa ni wale walioko Tanzania, Kenya, Somalia na Burundi.

Mafuriko katika nchi za Kenya na Tanzania yamepelekea watu wasiopungua 350 kufariki dunia na idadi hiyo inatazamiwa kuongezeka huku mvua zikilendelea kunyesha.