May 08, 2024 07:13 UTC
  • Iran na Oman zataka kukomeshwa haraka jinai za Israel Gaza

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman wametoa mwito wa kukomeshwa haraka iwezekanavyo jinai za utawala haramu wa Israel huko Gaza Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Badr bin Hamad Al Busaidi wa Oman wametoa mwito huo katika mazungumzo yao kwa njia ya simu.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Oman wamefanya mapitio ya matukio ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza juu ya udharura wa kukomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina, usitishaji vita mara moja, kuachiliwa huru wafungwa na kutumwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza.

Mawaziri wa Oman na Iran wamejadili matukio ya Gaza katika hali ambayo, jana utawala haramu wa Israel ulianzisha hujuma na mashambulio makubwa katika mji wa Rafah huuko Gaza Palestina na kuendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa maeneo hayo.

 

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yao hayo, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran  na Oman wamezungumzia mahusiano ya Tehran na Muscat  na kusisitiza umuhimu wa kuimarishwa na kupanuliwa zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili za Kiislamuu katika nyuga mbalimbali.

Aidha  Hussein Amir-Abdollahian na Badr bin Hamad Al Busaidi  wamesisitizia umuhimu wa kuendelezwa njia ya sasa ya kustawisha uhusiano kati ya mataifa hayo.