May 08, 2024 02:23 UTC
  • Eslami: Mienendo ya kiuhasama ya Israel isiathiri uhusiano wa Iran na IAEA

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema hatua na mienendo ya kiuadui ya utawala wa Kizayuni wa Israel haipasi kuathiri uhusiano na ushirikiano baina ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Mohammad Eslami aliyasema hayo jana Jumanne hapa Tehran katika mkutano wake na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), kuelekea Mkutano wa 30 wa Kitaifa wa Nyuklia wa Iran na mkutano wa kwanza wa kimataifa wa sayansi na teknolojia ya nyuklia.

Eslami amesisitiza kuwa: "Hatua za kiuhasama dhidi ya Iran, zenye mizizi ya Kizayuni, zinapaswa kutazamwa kwa makini, ili zisiathiri ushirikiano baina ya pande mbili."

"Dhati ya utawala wa Israel imeanikwa machoni pa dunia, na inaunga mkono mienendo ya kiuharibifu dhidi ya Iran," ameongeza Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran.

Kadhalika Eslami amepongeza mazungumzo yaliyokuwa na 'tija' baina yake na Grossi na kutaja taarifa ya pamoja iliyotolewa mwaka jana akiwa pamoja na mkuu huyo wa IAEA kuwa ramani ya njia ya kuimarisha ushirikiano baina ya Iran na wakala huo wa Umoja wa Mataifa.

Eslami na Grossi wakihutubia pamoja waandishi wa habari

Mapema jana pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, alisema katika mazungumzo yake na Grossi hapa Tehran kwamba, kwa kutilia maanani rekodi ya Marekani ya kuhalifu ahadi katika mikataba ya huko nyuma kuhusiana na mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) usiathiriwe na mtazamo na mwenendo usio thabiti na wenye migongano wa Washington.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amesisitiza kuwa, kuimarishwa mchakato wa ushirikiano kati ya Iran na wakala huo kutapelekea kushindwa pande zinazotaka kuzidisha migogoro, mivutano na makabiliano katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa kutumia visingizio vya aina mbalimbali.    

Tags