May 08, 2024 08:15 UTC
  • Harakati ya kimataifa ya mwamko wa wanafunzi wa vyuo vikuu dhidi ya Wazayuni

Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika kipindi cha leo cha Makala ya Wiki ambacho kinatupia jicho uasi na harakati ya maandamano na migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu Marekani na Ulaya wakipinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza. **** *****

Harakati ya mwamko ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani dhidi ya utawala katili wa Israel iliyoanzia katika Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York sasa imesambaa katika vyuo vikuu vya nchi nyingine duniani.

Maandamano ya amani ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Colombia, Marekani dhidi ya mauaji ya kimbari ya Israel Ukanda wa Gaza

Wiki mbili zimepita tangu kuanza kwa maandamano na migomo ya kupinga siasa za mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza katika vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya. Nchi za Magharibi zinakabiliana na maandamano hayo kwa ngumi ya chuma na ukandamizaji wa kikatili dhidi ya wanafunzi.

Kunyamaza kimya na kutochukua hatua  Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo kuhusiana na jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya binadamu huko Gaza kumewafanya wasomi na wanataaluma wa vyuo vikuu nchini Marekani, Ulaya na maeneo mengine ya dunia wasimame na kupinga vikali jinai hizo na kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya uhalifu huo. Vyombo vya habari duniani pia vimeakisi matukio ya ukandamizaji wa vyombo vya usalama kwenye vyuo vikuu katika nchi tofauti za Magharibi hususan Marekani. Picha na video za vyombo hivyo, ambazo zimekuwa mada kuu ya vyombo vya habari duniani kwa muda wa wiki mbili zilizopita, ni kielelezo cha wazi cha mtazamo na sera za kinafiki na kindumakuwili za nchi za Magharibi katika suala la demokrasia. Polisi na taasisi za usalama za nchi za Magharibi zimekabiliana na maandamano ya wanafunzi hao dhidi ya jinai za kivita za Israel na mauaji ya kimbari huko Gaza kwa kuwashambulia na kuwatia mbaroni.

Herbert Marcuse, mwanafalsafa  Mjerumani-Mmarekani (aliyezaliwa 1898-na kufariki dunia 1979) na mmoja wa waanzilishi wa Shule ya Frankfurt, alisema kuwa Marekani inaendeleza vita vyake dhidi ya watu kwa kaulimbiu za uhuru, ubinadamu na demokrasia, na kwamba taasisi za serikali ya Marekani zimekuwa chombo cha kukandamiza uhuru. Inaonekana kwamba kauli hii iliyotolewa na Marcuse miongo kadhaa iliyopita imepata dhihirisho la wazi na halisi, kwa sababu katika maandamano ya amani ya wanafunzi wa Marekani na kukandamizwa kwao na serikali kwa sababu tu ya kupinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza, uhuru wa kujieleza umekandamizwa na kukanyagwa kikamilifu.

Cheche ya mwanzo ya uasi huu ilijitokeza wakati wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani walipokusanyika kwenye kampasi ya Chuo Kikuu cha Columbia katika Jiji la New York mnamo Aprili 18 na kutangaza upinzani wao kwa vita vinavyofadhiliwa na nchi yao dhidi ya watu wa Gaza. Waandamanaji hao waliwataka wasimamizi wa vyuo vyao kusimamisha ushirikiano na vyuo vikuu vya Israel na kuondoa fedha na mitaji yao kwenye makampuni yanayounga mkono kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.

Maandmano ya kupinga vita Ukanda wa Gaza 

Baada ya jeshi la polisi kukamata makumi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Columbia, hasira zilienea katika vyuo vikuu vingine vya nchi hiyo na maandamano hayo yamepanuka na kugubika vyuo vikuu katika majimbo tofauti ya nchi hiyo. Harakati hiyo ya wanafunzi wa vyuo vikuu ya kuwatetea Wapalestina katika vyuo vikuu vya Marekani, imevuka mpaka na kusambaa katika vyuo vikuu vya nchi mbalimbali duniani kama Ufaransa, Uingereza, Austia na Ujerumani.

Uasi na maandamano ya wanafunzi wa Marekani na Ulaya ya kuwaunga mkono wakazi wa Gaza na takwa la kusimamishwa vita katika eneo hilo na kuyawekea vikwazo makampuni yanayotoa silaha kwa utawala wa Kizayuni, yamekuwa changamoto kwa serikali za nchi za Magharibi. Ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya amani ya wanafunzi wa vyo vikuu wa Kimarekani unaonyesha ni kwa kiasi gani jamii ya Kiyahudi inayounga mkono Uzayuni huko Marekani inahisi kutishiwa na maandamano hayo.  *****                                                                  *****

Msimamo wa taasisi na maafisa wa Kizayuni dhidi ya vuguvugu hilo la wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya wanaoandamana na kufanya mgomo kupinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel na kuwaunga mkono watu wa Gaza umekuwa wa kusikitisha na kufedhehesha. Shirika la Ujasusi la Israel, Mossad, linatoa vitisho dhidi wanafunzi hao, na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huu ametoa wito wa kukandamizwa wanafunzi hao. 

Uongozi wa vyuo vikuu vya Marekani pia umefuata sera ya serikali ya nchi hiyo na kuwakandamiza wanafunzi wanaoandamana, na kwa upande mwingine, wajumbe wa Congress wamemuomba Rais wa Marekani, Joe Biden, kutuma askari wa taifa kukabiliana na waandamanaji hao. Licha ya ukandamizaji na kutiwa mbaroni mamia ya wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu na kufukuzwa baadhi ya wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu vya kifahari vya Marekani, harakati za wanafunzi za kuwaunga mkono wananchi wa Palestina bado zinaendelea kupanuka.

Waandamanaji wanaoitetea Palestina katika Chuo Kikuu cha British Columbia mjini Vancouver pia waliweka mahema kwenye kampasi ya chuo hicho na kutaka yongozi wake kuondoa vitega uchumi katika taasisi na makampuni yenye uhusiano na Israel na kuuwekeka utawala hio vikwazo vya ushirikiano wa kitaaluma.

David Hearst, mchambuzi mashuhuri wa Kiingereza amelitaja wimbi la maandamano ya sasa dhidi ya Wazayuni katika vyuo vikuu vya Magharibi kuwa ni sawa na harakati za wanafunzi za miaka ya 1960 katika nchi za Magharibi wakipinga vita vya Vietnam. Hearst anasema: "Harakati za kupinga vita vya Gaza zimefufua mapambano ya kupigania ukombozi ya kitaifa ya Palestina." Anasisitiza kuwa: "Makundi ya ushawishi yanayoiunga mkono Israel yanawatuhumu wanasiasa wanaoitetea Palestina kuwa wana chuki dhidi ya Wayahudi.

David Hearst anasema: "Wanawalazimisha maafisa wenye hofu na woga wa vyuo vikuu kuwatimua maprofesa na wahadhiri wa vyuo vikuu kwa sababu tu ya kuwatetea Wapalestina, na licha ya kujiita wanademokrasia, lakini wanatumia mbinu za kifashisti. Wanahatarisha utawala wa sheria, uhuru wa kusema na haki ya kuandamana."    *****                                              *****

Tags