Apr 26, 2024 10:58 UTC
  • Afisa wa nne wa Wizara ya Mambo ya Nje ya US ajiuzulu kupinga sera kuhusiana na vita vya Ghaza

Msemaji wa kitengo cha Kiarabu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amejiuzulu wadhifa wake kulalamikia na kupinga sera za serikali ya nchi hiyo katika vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Wakati imeshapita miezi saba tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza, Marekani inaendeleza sera zake za kuunga mkono mauaji hayo yanayofanywa na utawala huo ghasibu.
 
Kwa sababu hiyo, hatua za Washington za kuongeza kila uchao misaada yake kwa Israel ili iweze kujinasua kwenye kinamasi cha vita vya Ghaza vilivyodumu kwa miezi saba sasa bila ya kuiletea mafanikio yoyote Tel Aviv, zimekosolewa vikali na maoni ya umma ndani ya Marekani kwenyewe.
 
Kwa mujibu wa IRNA, Hala Rharrit, msemaji wa kitengo cha Kiarabu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amejiuzulu wadhifa wake kupinga sera za serikali ya Rais Joe Biden kuhusiana na Ghaza.
 
Kabla ya hapo, maafisa wengine watatu wa Marekani nao pia walijiuzulu nyadhifa zao kupinga na kulalamikia uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni katika vita vya Ghaza.
Wawili juu na mmoja kushoto: Maafisa watatu wa serikali ya Marekani waliojiuzulu nyadhifa zao

Annelle Sheline, Afisa wa Uhusiano wa Nje katika Ofisi ya Marekani ya Demokrasia, Haki za Binadamu na Kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na Josh Paul, Afisa wa Masuala ya Kisiasa na Kijeshi wa wizara hiyohiyo, walijiuzulu nyadhifa zao kupinga misaada ya silaha inayotolewa na Washington kwa utawala wa Kizayuni ili uzitumie katika vita dhidi ya Wapalestina wa Ghaza.

 
Mwezi Januari mwaka huu, Tariq Habash, msaidizi maalumu wa Rais wa Marekani katika Wizara ya Elimu, alitangaza kujiuzulu wadhifa huo akilalamikia jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina.
 
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya Wapalestina 34,000 wameshauawa shahidi hadi sasa tangu vilipoanza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza Oktoba 7, 2023.../