Apr 27, 2024 02:48 UTC
  • Raisi: Mtazamo wa Iran kuhusu Afrika ni wa kimkakati na unaozingatia maslahi ya pamoja

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja mtazamo wa Iran kuhusu bara la Afrika kuwa ni wa kistratijia na unaozingatia maslahi ya pamoja na akasisitiza azma ya viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbili za Iran na Zimbabwe ya kupanua na kuboresha kiwango cha ushirikiano.

Sayyid Ebrahim Raisi, ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Constantino Chiwenga pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Iran na Afrika uliofanyika jana mjini Tehran. Amesisitiza mtazamo wa Iran wa kustawisha zaidi uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na nchi za Afrika na kusema, kushiriki katika mkutano huu na kutembelea maonyesho ya Iran Expo 2024 ni fursa adhimu sana ya kuwafahamisha maafisa wa bara la Afrika uwezo wa Iran katika sekta mbalimbali. Vilevile amesisitiza utayarifu wa Iran kubadilishana uwezo na nchi za Afrika.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Constantino Chiwenga ameashiria historia ndefu ya uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili hususan baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kutoa wito wa kuzidishwa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili kwa kutilia maanani uhusiano huo wa karibu na wa siku nyingi.

Chiwenga ameitaja sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu nchi za Kiafrika kuwa ya kimsingi na ya kuaminika na akasisitiza utayarifu wa nchi yake kuendeleza ushirikiano na Iran.

Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Iran na Afrika ulifanyika jana Ijumaa (Aprili 26, 2024) mjini Tehran ukihudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa nchi za Kiafrika wakiwemo mawaziri wa uchumi wa nchi zaidi ya 30 za Kiafrika.

Sayyid Ebrahim Raisi

Akifungua mkutano huo, Rais Ebrahim Raisi alisema: Hatua ya Wizara ya Biashara ya Iran ya kuandaa mkutano huo ni muhimu katika kuwezesha Waafrika kufahamu uwezo wa Iran na Wairani pia kufahamu uwezo wa Afrika.