Apr 27, 2024 02:47 UTC
  • Mbali na walionyofolewa viungo, Wapalestina wengine walizikwa wakiwa hai kwenye makaburi ya halaiki Ghaza

Wahudumu wa afya, timu za uokoaji na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanawashutumu askari vamizi wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuwanyofoa viungo Wapalestina na hata kuwazika baadhi yao wakiwa hai kwenye makaburi ya halaiki yaliyogunguliwa kwenye eneo la karibu na Hospitali ya Nasser huko Ukanda wa Ghaza, baada ya askari hao katili kuondoka katika eneo hilo Aprili 7 kufuatia mashambulizi ya ardhini ya miezi minne.

Wahudumu wa afya na timu za uokoaji zilizoshiriki katika zoezi la ufukuaji miili ya raia Wapalestina waliozikwa kwenye makaburi ya umati yaliyogunduliwa kwenye eneo la Hospitali ya Nasser huko Khan Younis kusini mwa Ghaza wameripoti kuwa jeshi la Israel limehusika na wizi wa viungo; na kwamba baadhi ya Wapalestina hao walizikwa wakiwa hai kwenye makaburi hayo yaliyogunduliwa hivi majuzi.
 
Miili ipatayo 392, ikiwemo 165 ya watu ambao wameshindwa kutambuliwa imefukuliwa hadi sasa kutoka kwenye makaburi matatu ya halaiki baada ya askari wa jeshi katili la Israel kuondoka huko Khan Younis.
 
Ushahidi wa kutisha wa mateso, ikiwa ni pamoja na watu hao kufungwa kamba za plastiki na kuharibiwa makusudi sura zao ili wasitambuliwe umefichuka kupitia kwenye mikanda ya video na picha za wahasiriwa.
Timu za uokoaji zikiendelea na zoezi la ufukuaji maiti kwenye makaburi ya umati

Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Human Rights Monitor lilitangaza mapema wiki hii kuwa, lina wasiwasi kwamba kuna uwezekano umefanyika wizi wa viungo vya maiti za Wapalestina, kufuatia ripoti zilizotolewa na wataalamu wa afya huko Ghaza ambao walichunguza baadhi ya miili baada ya kuachiliwa na jeshi la Israel.

 
Shirika hilo lisilo la kiserikali limesema limerekodi taarifa kuhusu wanajeshi wa Israel waliochukua makumi ya maiti za Wapalestina katika hospitali za Al Shifa na Indonesia kaskazini mwa Ghaza, mbali na nyingine za kusini mwa eneo hilo.
 
Mapema wiki hii, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa umoja huo Volker Turk alisema "ameshtushwa" na uharibifu uliofanywa kwenye Hospitali ya Nasser na Hospitali ya Al Shifa pamoja na taarifa za kugunduliwa makaburi ya halaiki karibu na maeneo hayo na kutaka uchunguzi "huru, madhubuti na wa uwazi" ufanyike juu ya vifo hivyo.
 
Mbali na nchi kadhaa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) nayo pia imetoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita uliofanywa na jeshi la Israel katika Hospitali ya Nasser huko Ghaza, ambapo mamia ya miili ya raia inaendelea kupatikana kwenye makaburi ya umati.../

Tags