Apr 26, 2024 14:37 UTC
  • Kikao cha Pili cha Kimataifa cha Iran na Afrika; nembo ya azma ya kupanua ushirikiano

Kikao cha pili cha kimataifa kati ya Iran na Afrika kimefanyika leo asubuhi (Ijumaa) kwa kuhudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa masuala ya kiuchumi wa nchi zaidi ya 30 za Afrika na kwa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ukumbi wa mikutano wa nchi za Kiislamu mjini Tehran.

Akihutubia katika mkutano huo, Raisi Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuna irada baina ya Iran na Afrika ya kuimarisha na kustawisha uhusiano wa kibiashara.

Ameongeza kuwa: Hatua ya kwanza baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Bara la Afrika ni irada na kwamba, la kumshukuru Mwenyezi Mungu ni kwamba, irada na azma ipo na kikao hiki ni ishara ya azma ya nchi za Kiafrika na Iran ya kupanua uhusiano wa kiuchumi.

Utendaji wa serikali ya awamu ya 13 ya Iran ni kupanua uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na nchi za bara la Afrika hususan nchi za Kiislamu za bara hilo. Katika fremu hii, rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka jana alifanya safari kwa mwaliko rasmi wa marais wa Kenya, Uganda na Zimbabwe, na katika safari hiyo ya siku 3, jumla ya hati 21 za ushirikiano zilitiwa saini. Mwezi uuliopita wa Machi pia Ebrahim Raisi alikwenda Algiers, mji mkuu wa Algeria, ambapo aliuongoza ujumbe wa kiuchumi na kisiasa wa Iran akiitikia mwaliko wa rais wa nchi huyo Abdelmajid Tebboune.

Kwa utendaji huu wa serikali ya awamu ya 13 ya Iran, mpango wa maendeleo wa mauzo ya nje ya bidhaha zisizo za mafuta na upanuzi wa uhusiano wa kibiashara na Afrika uliongezeka, na katika miaka miwili iliyopita, jumbe rasmi zaidi ya hamsini kutoka Afrika zimefanya safari hapa Iran na kutiwa saini mikataba mbalimbali. Pamoja na hayo, licha ya kuwa, kiwango cha biashara kati ya Iran na nchi za Afrika kimekuwa kikiongezeka wakati fulani, lakini ni mbali na lengo la dola bilioni 10. Hivi sasa, uingizaji wa bidhaa hapa nchini kutoka Afrika umetangazwa kuwa ni karibu dola bilioni 600, lakini hisa ya Iran katika kiasi hiki haifiki hata dola bilioni 2. Hii ni katika hali ambayo, nyuga za ushirikiano na ongezeko la uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Afrika ni muhimu hususan katika nyanja za nishati, uhandisi wa kiufundi, uchukuzi, kilimo na madini.

Mjumbe wa Umoja wa Afrika Patrick Lalande akihutubu katika kikao cha Iran na Afrika jijini Tehran

 

Kwa hivyo, Shirika la Maendeleo ya Biashara la Iran lina mipango ya kuchukua hisa kubwa ya soko la bara la Afrika. Katika fremu hiyo hiyo, Abbas Aliabadi, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran amesisitiza juu ya kuanzishwa kwa sekretarieti ya kudumu ya Kikao cha Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika katika wizara hii na kufuatilia masuala muhimu kwa ajili ya kupanua mahusiano na nchi za Afrika.

Hivi sasa kuna mipango ya maendeleo ya biashara, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya miundombinu, kutatua matatizo yanayohusiana na mahusiano ya kibenki na kuongeza ushirikiano wa kutatua matatizo kwa sura ya kiduru. Kwa hakika haya ni miongoni mwa masuala ambayo yapo katika ajenda za viongozi wa Iran na Afrika.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inajaribu kupanua mabadilishano ya kibiashara kupitia kuendeleza njia za meli hadi Afrika Magharibi na Kusini na kutoa huduma zenye mpangilio kwa mashirika ya ndege kutoa kipaumbele kwa nchi moja au mbili katika kila eneo kwa kutumia uwezo na tajiriba ya uchukuzi na usafiri.

ukumbi wa mikutano wa nchi za Kiislamu mjini Tehran

 

Katika hali hii, inapasa kuzingatia kwamba, kupanua ushirikiano na nchi za Kiafrika pia ni muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mtazamo wa kisiasa, kwa sababu kuna nchi 30 za Kiislamu katika bara hilo na karibu 50% ya wakazi wake ni Waislamu. Pia, nchi 50 kati ya 54 za bara hilo ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).

Inatazamiwa kuwa, kutokana na kuwepo maafisa wa juu wa kiuchumi na kibiashara wa nchi za Kiafrika katika mkutano wa pili wa kimataifa wa Iran na Afrika, mikataba mizuri itatiwa saini baina ya pande hizo mbili na hivyo kupigwa hatua moja mbele kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Tags