May 07, 2024 11:26 UTC
  • Amnesty International: Mashambulizi ya anga ya Somalia yaliwaua raia

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema kuwa, mashambulizi mawili ya anga yaliyofanywa na jeshi la Somalia yaliwaua raia 23 mnamo mwezi Machi mwaka huu.

Hayo yamo katika ripoti ya Amnesty Internationa ambao inaeleza kuwa, mashambulizi hayo yalifanywa kwa kutumia droni zilizoundwa nchini Uturuki.

Aidha taarifa hiyo inasema kuwa, mashambulizi hayo ya Machi 18 yalililenga shamba moja karibu na kijiji cha Bagdad, kilicho mkoa wa kusini mwa Somalia wa Lower Shabelle.

Shirika hilo limetoa mwito wa uchunguzi huru wa mkasa huyo ikiwemo iwapo kile kilichotokea kinaweza kuorodheshwa kama "uhalifu wa kivita".

Wachunguzi wa Amnesty waliwahoji watu 12, wakiwemo manusura na mashahuda ambao wamesema mashambulizi hayo ya droni yalifuatiwa na mapigano ya ardhini kati ya Al Shabaab ma vikosi vya serikali.

 

Ikitumia ushahidi kutoka kwa wakaazi na manusura pamoja na tathmini ya picha za satelaiti na picha za mabaki ya mabomu, Amnesty International imefanikiwa kubaini kwamba shambulio hilo lilifanywa na vikosi vya Somalia. Shirika hilo limedai mabomu yaliyotumika pamoja na droni chapa TB-2 vyote vimeundwa Uturuki na vikosi vya Somalia hutumia aina hiyo ya silaha.

Mohamed Ali Deerey, ambaye mashambulizi hayo yaliwaua mdogo wake wa kiume na mpwa wake aliyekuwa na umri wa miaka 9, ameliambia shirika la Amnesty kwamba alifika shambani muda mfupi tu baada kusikia shambulio la kwanza. Amesema muda mfupi baadaye shambulio la pili lilipiga eneo hilo na kusababisha vifo vya watu wengi zaidi.