May 05, 2024 06:45 UTC
  • Irani, Misri zinajadili kukuza uhusiano, kukomesha ukatili wa Israel

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Misri wamejadili njia zinazowezekana za kustawisha uhusiano wa pande mbili na kukomesha jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian na mwenzake wa Misri, Sameh Shoukry walikutana jana katika mji mkuu wa Gambia, Banjul, kando ya mkutano wa 15 wa kila mwaka wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na kusisitiza kwamba serikali za Iran na Misri zimeazimia kuimarisha uhusiano wa pande zote.

Walibadilishana mawazo kuhusu matukio ya sasa hususan vita vya mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza na kueleza matumaini yao kuwa mkutano huo wa OIC utaimarisha mshikamano na umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu ili kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kutatua migogoro ya kieneo.

Mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Misri, Banjul

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza jitihada za Misri za kusitisha mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na kuiomba Cairo kuisaidia Tehran kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu waliokumbwa na vita katika ukanda huo.

Takriban Wapalestina 34,654, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, wameuawa na 77,908 kujeruhiwa katika vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.

Tags