May 07, 2024 11:27 UTC
  •  Mamilioni hawana chakula mataifa matatu kanda ya Sahel

Shirika la Kimataifa la Msaada wa Kibinadamu la International Rescue Committee (IRC) limetangaza kuwa, idadi ya watu wanaotaabika kutokana na ukosefu "mkubwa" wa chakula kwenye mataifa matatu ya kanda ya Sahel imefikia milioni 7.5.

Taarifa ya shirika hilo inasema kuwa, kiwango cha ukosefu wa chakula kwenye nchi za Mali, Burkina na Niger kimezidi kuongezeka ikiwa ni pamoja na visa chungu nzima vya utapiamlo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwenye mataifa hayo matatu yaliyo chini ya tawala za kijeshi, idadi hiyo ya watu milioni 7.5 imepanda kutoka milioni 5.4 mwaka uliopita wa 2023.

IRC imetahadharisha hali kama hiyo inaweza pia kusambaa kwenye mataifa mengine ya Cameroon, Chad na Nigeria iwapo hakutakuwa na mavuno ya kutosha ya chakula mwaka huu.

 

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umewahi kutangaza katika ripoti yake kuwa watoto milioni 10 katika eneo la Sahel barani Afrika, ikiwa ni pamoja na Burkina Faso, Mali na Niger, wanaishi katika mazingira hatarishi, huku idadi ya watoto hao ikiwa imeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka 2020.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, watoto katika maeneo ya Pembe ya Afrika na Sahel wako kwenye tishio kubwa la kupoteza maisha kwa wingi iwapo msaada wa haraka hautatolewa, huku utapiamlo mkali na hatari ya magonjwa ya kuambukiza kutokana na kukosa maji safi ya kunywa, yakizidi kuwa makubwa.