May 07, 2024 02:14 UTC
  • Utayari wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran wa kuendesha duru ya pili ya Uchaguzi wa Bunge

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran ametangaza utayarifu wa wizara hiyo wa kuendesha duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) siku ya Ijumaa ya tarehe 10 Mei.

Ahmad Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Iran amethibitisha kuwa maandalizi yamekamilika kwa ajili ya kuendesha duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge la 12 mnamo siku ya Ijumaa ya tarehe 10 Mei na kusema kuwa, kwa mara ya kwanza uchaguzi huo utafanyika kikamilifu kielektroniki katika majimbo manane ya uchaguzi ambayo ni Tehran, Tabriz, Abadan, Shiraz, Kermanshah, Khorramabad, Qaimshahr na Malair.

Duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu itafanyika katika mikoa 15 nchini na kwa ajili hiyo, vimetengwa vituo 11,500 vya kupigia kura katika maeneo 22 ya uchaguzi.

Utayari wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa kuendesha duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge 

 

Kwa muktadha huo, kampeni za wagombea zilianza rasmi siku ya Alkhamisi ya tarehe Pili Mei na zitaendelea kwa muda wa wiki hadi siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika eneo la mji wa Tehran, ulifanyika mchuano kati ya wagombea 3,372, ambapo wagombea 14 kati ya hao walipata kura za kutosha kuingia bungeni, na wengine 16 watapatikana siku ya Ijumaa ijayo katika duru ya pili ya uchaguzi huo.

Uchaguzi wa Bunge la 12 na wa Baraza la sita la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu ulifanyika kwa wakati mmoja kote nchini Iran siku ya Ijumaa ya tarehe Mosi Machi kwa ushiriki wa wananchi wa matabaka mbalimbali.

Ijumaa tarehe 10 Mei, siku ya kufanyika duru ya pili ya Uchaguzi wa Bunge

 

Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ina wawakilishi 290 na idadi ya wawakilishi wa kila mkoa inatofautiana kutegemea na idadi ya watu wa mkoa husika.

Kwa mujibu wa Ibara ya 62 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baada ya kuthibitishwa kuwa na sifa za kugombea, wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi, na hutumikia nafasi ya ubunge kwa kipindi cha miaka minne.

 Katika Bunge la Iran, kila moja kati ya jamii za Wazartoshti na Wayahudi huchagua mwakilishi wao mmoja, Wakristo wa Assyrian na Chaldean wao huwa na mwakilishi mmoja wa pamoja, na kila moja kati ya jamii ya Wakristo wa Armenia wa kusini na kaskazini huchagua mwakilishi wao mmoja.

Kwa maelezo hayo, Ijumaa ya tarehe 10 Mei, wananchi wa Iran wataelekea tena vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuendeleza malengo yao matukufu na mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa mstari wa mbele katika mfumo wa utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi, na kwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura, wananchi wa Iran wamekuwa na nafasi kuu katika uendeshaji nchi.

Wakati huo huo, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ina nafasi na mchango muhimu sana katika muundo wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa sababu ndiyo inayotunga sheria na kusimamia utendaji wa Baraza la Mawaziri kutokana na mamlaka iliyonayo ya kuwaidhinisha kwa kuwapigia kura ya kuwa na imani nao wale wote wanaopendekezwa kushika nyadhifa za utendaji Serikalini.

Kwa sababu hiyo, wananchi wa Iran daima hujitokeza kwa wingi katika upigaji kura ili mbali na kuonyesha uaminifu wao kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kutoa mchango wao pia wa Kimapinduzi na Kiislamu katika uundaji wa bunge imara na lenye uwezo madhubuti.

Kama alivyoeleza Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba Bunge lina nafasi kuu ya uendeshaji mambo katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuwepo maelfu ya wagombea katika mchuano wa uchaguzi kunatoa fursa nyingi kwa wapigakura za kuchagua ili kuhakikisha Bunge la 12 la Iran linaundwa na wabunge wenye uweledi wa uendeshaji mambo.

 

Tags