Apr 26, 2024 07:53 UTC
  • Iran inatoa wito kwa BRICS kuchukua jukumu kukomesha jinai za Israel

Iran imetoa wito kwa kundi la BRICS la mataifa yanayoinukia kiuchumi kuchukua jukumu la kukomesha mara moja jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Wito wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani mjini Moscow siku ya Alhamisi umekuja wakati wenzake na wawakilishi maalum wa mataifa ya BRICs walipokutana kujadili maendeleo ya hivi punde katika eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini.

Nchi wanachama wa BRICS ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini pamoja na Iran, Imarati, Misri na Ethiopia

Bagheri Kani ametoa wito kwa mataifa ya BRICS kusaidia katika kupeleka haraka misaada ya kibinadamu, hasa chakula, vifaa vya matibabu na dawa katika Ukanda wa Gaza na kuchukua hatua za kuhakikisha wanajeshi vamizi wa Israel wanaondoka eneo hilo sambamba na kuanza mkakati wa kulijenga upya.

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran ameishukuru Afrika Kusini kwa kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Amewataka wanachama wa BRICS kuunga mkono kwa dhati kesi hiyo na kutoa masuluhisho ya kisheria yanayohitajika ili kukabiliana na utawala huo unaotenda jinai wa Israel.

Bagheri Kani amesema "msingi wa kuanzishwa utulivu na amani katika eneo kutoka Lebanon hadi Iraq na Bahari ya Sham ni kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi wala makazi wa Gaza."

Amegusia jaribio la Wamagharibi la kuhalalisha jinai za Israel dhidi ya binadamu chini ya kanuni ya haki ya kujilinda na kusema, "uhalali huu wa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni ni batili kabisa kwa mtazamo wa kisheria na kimataifa".

Bagheri Kani pia amegusia shambulio la Israel dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kuuawa shahidi makamanda wa kijeshi wa Iran na wafanyakazi katika jengo hilo.

Amesema baada ya jinai hiyo isiyokuwa na kifani na iliyo kinyume cha sheria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitumia haki yake ya kujilinda kisheria na hivyo kuupa utawala ghasibu wa Israel jibu kali kutokana na jinai zake huko Damascus.