Apr 26, 2024 07:41 UTC
  • Vikosi vya Yemen vyashambulia meli ya Israel, Bandari ya Eilat kuonyesha mshikamano na Gaza

Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimefanikiwa kulenga meli ya utawala wa Israel katika Ghuba ya Aden pamoja na Bandari ya Eilat katika sehemu ya kusini ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) katika operesheni mpya zinazoiunga mkono Palestina.

Msemaji wa vikosi hivyo Brigedia Jenerali Yahya Saree alitangaza operesheni hiyo katika taarifa ya video siku ya Alhamisi.

Alitaja meli iiliyolengwa kuwa ni "MSC Darwin," na kubainisha kuwa meli hiyo ya mizigo ya Israel ililengwa kwa  makombora na ndege zisizo na rubani ambapo ameitaja operesheni hiyo kuwa iliyofanikiwa.

Jenerali Saree amesema vikosi vya Yemen pia vimerusha "makombora kadhaa ya balestiki na ya cruise ambayo yamelenga maeneo kadhaa ya "Israel" katika Bandari ya Eilat.

Kauli hiyo imekuja siku moja tu baada ya msemaji huyo kutangaza kuwa vikosi hivyo vimelenga meli mbili za Marekani, moja ya mizigo na nyingine ya kivita na pia meli moja ya mizigo ya  Israel katika kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambao wanavumilia vita vya mauaji ya kimbari vinavyoungwa mkono na Marekani.

Wizara ya Afya Gaza inasema zaidi ya wapalestina 34,000 wameuawa shahidi Gaza na zaidi ya 77,000 wamejeruhiwa, wengi wakiwa ni wanawke na watoto tangu Israel ianzishe vita dhidi y Gaza Oktoba mwaka jana.

Mashambulizi katika Bahari ya Sham yanayotekelezwa na majeshi ya Yemen yamelazimisha baadhi ya makampuni makubwa ya meli za biashara na mafuta kusimamisha usafiri kupitia mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya baharini.

Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimesema havitakomesha mashambulizi ya kulipiza kisasi hadi mashambulizi ya anga na nchi kavu ya Israel huko Gaza, yatakapokoma.