Sep 22, 2023 02:44 UTC
  • Baqeri: Ghuba ya Uajemi inahitaji usalama wa nchi za eneo tu

Mkuu wa Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa uwepo wa kijeshi wa maajinabi katika Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kuwa, nchi za eneo hili zina uwezo wa kujidhaminia usalama wao.

Meja Jenerali Mohammad Hossein Baqeri amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Tasnim na kuongeza kuwa, "Tunaamini kuwa, usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi lazima udhaminiwe kupitia ukuruba na ushirikiano wa mataifa ya eneo hili."

Mkuu wa Majeshi ya Iran alisema hayo jana Alkhamisi hapa Tehran katika mazungumzo yake na Kamanda wa Jeshi la Utawala wa Kifalme wa Oman, Meja Jenerali Matar bin Salim bin Rashid al Balushi na kubainisha kuwa, usalama wa Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari Hindi hauna mfungamano wowote na maajinabi, na kwamba nchi za eneo zina uwezo wa kujidhaminia usalama wao.

Ameeleza bayana kuwa, mataifa ya eneo hili la kistratajia yana uwezo wa kuhakikisha kuwa kuna uthabiti na usalama wa kutosha katika nchi za eneo, pasi na kutegemea uwepo na uingiliaji wa vikosi vya kigeni.

Meja Jenerali Mohammad Hossein Baqeri aidha ameashiria uwezo mkubwa wa majeshi ya Iran na Oman katika nyuga za operesheni, mafunzo na intelijensia na kubainisha kuwa, kubadilishana uzoefu baina ya nchi mbili hizi kutaimarisha usalama wa eneo zima.

Ramani inayoonesha Ghuba ya Uajemi

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Utawala wa Kifalme wa Oman, Meja Jenerali Matar bin Salim bin Rashid al Balushi amesisitizia haja ya kuimarishwa ushirikiano wa kijeshi baina ya Muscat na Tehran.

Aidha wawili hao wamejadili njia za kustawisha uhusiano wa kiulinzi na kijeshi wa pande mbili. Kadhalika wamegusia masuala kama ya kupambana na ugaidi, kuimarisha usalama katika eneo hili na kutafuta njia za kupambana na ukosefu wa utulivu katika eneo hili kwa kustafidi vizuri na uzoefu na uwezo wa kiteknolojia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags