Wasudan 31 wauawa katika shambulio la RSF mjini Omdurman
Raia wasiopungua 31 wa Sudan wakiwemo watoto wameuawa na wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika mji wa Omdurman, kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan Khartoum.
Watoto wadogo walikuwa miongoni mwa wahanga wa hujuma hiyo katika eneo la Al-Salha mjini humo, Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulisema hayo jana Jumapili, ukisema mauaji hayo "ndiyo makubwa zaidi yaliyorekodiwa katika eneo hilo."
Mtandao huo umesema kuwa, waliouawa walituhumiwa na kundi hilo la wanamgambo kwamba walikuwa na mfungamano na jeshi la Sudan.
Wanaharakati wamesambaza video kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha watu binafsi waliovalia sare za RSF wakipiga risasi kundi la watu katika kitongoji cha Al-Salha. Mtandao huo umeuita umwagaji damu wa wanamgambo wa RSF "uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu."
Imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuwaokoa raia waliosalia kwa kufungua njia salama ili kuhakikisha wanatoka katika kitongoji cha Al-Salha. Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa kundi la waasi juu ya ripoti hiyo.
Shambulio hili ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi ya hivi karibuni ya ndege zisizo na rubani zilizolenga vituo vya umeme katika miji ya kaskazini mwa Sudan, ikiwa ni pamoja na Merowe, Dongola, Al Dabbah na Atbara.
Siku chache zilizopita, Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulisema watu 11 wameuawa na 22 kujeruhiwa wakati ndege isiyo na rubani ya Rapid Support Forces (RSF) iliposhambulia kambi ya wakimbizi huko Atbara, kaskazini mwa Sudan.