RSF ya Sudan yafanya mauaji mengine ya kutisha El-Fasher, Darfur Kaskazini
Raia wasiopungua 47 wameuawa katika mashambulizi ya mizinga yalilofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) huko El-Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini magharibi mwa Sudan.
Taarifa ya Jeshi la Sudan imesema kuwa, kundi hilo la waasi liliendelea na "mashambulizi ya kiholela" dhidi ya ya mji huo, na kufyatua takriban mizinga 250 katika vitongoji vya El-Fasher.
Wanawake kumi ni miongoni mwa wahanga wa shambulio hilo, huku makumi ya raia wakijeruhiwa na kuhamishiwa hospitali, imesema taarifa hiyo.
Jeshi la Sudan limeeleza bayana katika taarifa hiyo kuwa, vikosi vyake vimeharibu hifdhi ya makombora ya RSF huku kaskazini mwa El-Fasher. RSF haijatoa taarifa yoyote kuhusu mashambulizi hayo mapya na operesheni ya Jeshi la Sudan ya kuharibu silaha za kundi hilo.
Alkhamisi iliyopita, Jeshi la Sudan lilitangaza kuwa raia 62, wakiwemo watoto 15, waliuawa na wengine 75 kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora ya RSF katika maeneo mbalimbali ya El Fasher.
Aidha mapema wiki hii, kundi hilo la wanamgambo lilidai kutwaa udhibiti wa kambi ya wakimbizi ya Zamzam iliyoko El-Fasher baada ya makabiliano na vikosi vya jeshi. Takriban raia 400 waliuawa huku wengine zaidi ya 400,000 wakikimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Haya yanajiri huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) likifichua kuwa, mtu mmoja kati ya watatu nchini Sudan amelazimika kuwa mkimbizi, huku mamia ya watu wanaokimbia kambi za Darfur wakikabiliwa na hali mbaya kufuatia mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).