Wanaharakati Sudan: RSF imeua watu 300 Kordofan Kaskazini
Wanaharakati wa Sudan wamesema Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kimeua karibu watu 300 katika wimbi jipya la mashambulizi katika jimbo la Kordofan Kaskazini, magharibi mwa nchi.
Kundi la kutetea haki za binadamu la ‘Wanasheria wa Dharura’ lilisema katika taarifa yake jana Jumatatu kwamba, RSF imeshambulia vijiji kadhaa tangu siku ya Jumamosi karibu na mji wa Bara, ambao wanamgambo hao wanaudhibiti.
Wanaharakati hao wameeleza kuwa, katika kijiji kimoja huko Shag Alnom, zaidi ya watu 200 waliuawa kwa kuchomwa moto au kupigwa risasi siku ya Jumamosi.
Kadhalika wamesema mashambulizi mengine yaliyoandamana na uporaji katika vijiji vingine kadhaa vya jimbo hilo siku hiyo hiyo yaliua watu 38, huku makumi ya wengine wakitoweka.
Siku ya Jumapili, kundi hilo la wanasheria limesema, RSF ilishambulia kijiji cha Hilat Hamid na kuua watu 46, wakiwemo wajawazito na watoto. Zaidi ya watu 3,400 walilazimika kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Jimbo la Kordofan Kaskazini limekuwa likishuhudia ongezeko la mashambulizi tangu mapigano makali kati ya jeshi la kitaifa la Sudan na waasi wa RSF yalipozuka mwezi Aprili 2023.
Vita hivyo tayari vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 na kuwafanya watu milioni 14 kuhama makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za ndani nchini Sudan. Hata hivyo, tafiti huru zinaonyesha idadi ya waliopoteza maisha inaweza kupindukia watu 130,000.