UN: Ukatili unaofanyika Sudan hauna mipaka; vifo vyaongezeka Darfur
-
Volker Turk
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 540 wameuawa huko Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan katika muda wa wiki tatu zilizopita, huku wanajeshi wakizidisha opereseheni zao za kuukomboa mji wa el-Fasher, makao makuu ya jimbo hilo.
"Ukatili unaofanyika nchini Sudan hauna kikomo," Volker Turk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema katika taarifa yake kuhusu athari mbaya za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili.
Ripoti hiyo iliyotolewa jana Alhamisi ya UN imeeleza kuwa, kuna uwezekano mkubwa idadi ya vifo iliyotangazwa ya watu 542 katika wiki tatu zilizopita, ikawa ni "kubwa zaidi".
Darfur umekuwa uwanja mkuu wa mapigano katika vita vya kikatili vilivyozuka Aprili 2023 kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu, na kuwafanya wengine zaidi ya milioni 12 kuwa wakimbizi; huku Umoja wa Mataifa ukisema mgogoro huo ndilo janga baya zaidi la kibinadamu duniani.
RSF, ambayo ilipoteza Khartoum mwezi uliopita, katika wiki za hivi karibuni imefanya mashambulizi mengi dhidi ya el-Fasher na kambi za wakimbizi za karibu za Zamzam na Abu Shouk, na kusababisha mamia ya maelfu ya watu kuhamia mji wa Tawila.

Ikulu ya Rais wa Sudan katikati mwa Khartoum ilishambuliwa kwa makombora jana Alkhamisi na RSF, chanzo cha kijeshi kililiambia shirika la habari la AFP, shambulio la pili la aina hiyo katika mji mkuu ndani ya wiki moja.
Kauli ya Turk imekuja wakati RSF inakaribia kutwaa udhibiti wa mji wa kimkakati wa al-Nahud huko Kordofan Magharibi, lango la eneo la Darfur, linalodhibitiwa na jeshi la Sudan tangu kuanza kwa vita hivyo.