Hakim: Vikosi vya Hashdu Shaabi ni nguzo ya usalama wa Iraq
-
Ammar al-Hakim
Kiongozi wa Harakati ya Hikma ya Kitaifa ya Iraq, Ammar al-Hakim amevipongeza vikosi vya Hashdu Shaabi na kusisitiza kuwa vimekuwa na mchango mkubwa kwa usalama wa Iraq.
Wakati wa ziara yake ya karibuni katika Kamandi ya Operesheni ya harakati hiyo ya kujitolea wananchi wa Iraq katika Mkoa wa Anbar, katikati ya Iraq, Hakim alisema, "Hashdu Shaabi na vikosi vingine vya usalama vilijitolea kuushinda ugaidi na kuleta utulivu nchini Iraq."
Amevipongeza na kuvishukuru vikosi hivyo kwa kujitolea kwao muhanga kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo ya Kiarabu kutokana na tishio la ugaidi, na kuhakikisha kuwa utulivu unarejea katika maeneo yote ya nchi.
Kadhalika ametoa wito wa uwekezaji katika teknolojia mpya, ikiwa ni pamoja na Akili Mnemba (AI), ili kuimarisha usalama na uwezo wa kijasusi wa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Kadhalika Kiongozi wa Harakati ya Hikma ya Kitaifa ya Iraq amesisitiza kuwa, "wakati umewadia wa kuwa na nchi yenye mamlaka kamili ya kujitawala kwa kutokuwepo ndani yake askari wowote wa kigeni."
Sheikh Ammar al-Hakim ameeleza bayana kuwa, "Kulinda sifa na hadhi ya Hashdu Shaabi ni jukumu la kila mmoja. Maafisa wa serikali lazima washirikiane kwa uwazi katika masuala ya wananchi."
Ikumbukwe kuwa, mwaka 2014, Kiongozi na Marjaa wa Waisalmu wa Madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali Sistani alitoa fatwa na kuwataka wananchi wa Iraq kujiunga na safu za wanajeshi wa nchi hiyo kupambana na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).