Maelfu ya Waomani na Walibya waandamana kuunga mkono Palestina + Video
Maelfu ya wananchi wa Oman wamefanya maandamano kulaani jinai za utawala wa Kizayuni na kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina.
Shirika la habari la IRNA limeripoti leo Jumamosi kwamba, maelfu ya wananchi Waislamu wa Oman wameandamana na kukusanyika mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Muscat kulaani jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na utawala katili wa Israel huko Ghaza Palestina.
Wananchi wa Oman wametaka kukatwa uhusiano wa nchi yao na Marekani kwa sababu ndiye muungaji mkono mkuu wa jinai za Israel huko Palestina.
Katika upande mwingine, maelfu ya wananchi wa Libya, jana Ijumaa walimiminika mitaandi kwenye mji wa Misrata kutangaza hasira zao kutokana na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina hasa Ghaza.
Waandamanaji hao wamebeba bendera za Palestina na mabango yaliyoandikwa aya za Qur'ani Tukufu za kuhimiza kushikamana na Wapalestina na wamelaani dhulma wanayofanyiwa na Israel kwa kushirikiana na madola ya Magharibi hasa Marekani.
Waandamanaji hao wa Libya wameelezea hali ya Ghaza hivi sasa kuwa ni janga la kibinadamu kutokana na Israel na maadui wengine kutumia njaa kama silaha ya kuwaadhibu wananchi wa kawaida wa ukanda huo.
Wamesema kuwa vitendo hivyo ni ukiukaji wa wazi kabisa wa ubinadamu, sheria za kimataifa na ni uangamizaji wa kizazi.