Apr 25, 2024 07:27 UTC
  • Maandamano dhidi ya Netanyahu yageuka kuwa ya ghasia

Maandamano ya kupinga baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu huko Tel Aviv yageuka kuwa ya ghasia na vurugu kali.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRNA, walowezi wa utawala wa  Kizayuni wamekusanyika mbele ya makaazi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu usiku wa kuamkia leo, wakitaka wafungwa waachiliwe huru mara moja na kutiwa saini makubaliano ya mara moja ya usitishaji vita na Harakati ya Muqawama (Hamas) wa  Palestina (Hamas) katika Ukanda wa Gaza.

Familia za mateka wa utawala huo pia zimepiga nara dhidi ya Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa haramu wa Israel, hali ambayo imegeuka kuwa ghasia na vurugu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mazungumzo kuhusu usitishaji vita kati ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) na utawala haramu wa Kizayuni yamekwama ambapo mapendekezo yaliyopendekezwa hayajaafikiwa na pande zote mbili zinazohusika katika mgogoro huo.

Maandamano dhidi ya Netanyahu mjini Tel Aviv

Kukwama mazungumzo na kutofikiwa tija ni kwa maslahi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni, ambaye anataka kurefushwa vita kwa kuhofia kesi na kufunguliwa mashtaka dhidi yake kuhusiana na mauaji ya halaiki anayoyaendeleza huko Gaza.

Katika kivuli cha jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, Hamas haitaki kufanya mazungumzo na wahalifu waliohusika na jinai hizo na sasa wanawashinikiza wapatanishi waushinikize utawala huo ili uainishe wakati maalum wa kuanza mazungumzo jadi au faili la mazungumzo hayo lifungwe kabisa.

Tangu tarehe 7  mwezi Oktoba 2023, na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala ghasibu wa Kizayuni ulianzisha mauaji makubwa ya umati katika Ukanda wa Ghaza dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina, huku kimya cha jumuiya ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu kikiendelea kuonyesha unafiki na undumakuwili wa nchi hizo kuhusu jinai za utawala huo ghasibu na hivyo kuupa kiburi cha kuendelea kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wasio na hatia na hasa wanawake na watoto huko Gaza.

Tags