Apr 25, 2024 11:43 UTC
  • Wanachuo zaidi ya 100 wakamatwa California na Texas, US kwa kupinga vita vya Israel Ghaza

Polisi nchini Marekani wamewakamata makumi ya wanachuo walioandamana katika Chuo Kikuu cha Texas huko Austin (UT Austin) na Chuo Kikuu cha Kusini mwa California (USC) huku maandamano yanayoongozwa na wanafunzi kupinga vita vya Israel dhidi ya Ghaza yakizidi kushika kasi nchini kote naye Spika wa Bunge Mike Johnson akipendekeza kuombwa msaada wa askari wa Gadi ya Taifa.

Ukandamizaji na utiaji nguvuni huo wa wanachuo uliofanyika jana Jumatano katika miji ya Austin na Los Angeles kumejiri wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Harvard na Chuo Kikuu cha Brown kwenye pwani ya mashariki pia wamekaidi vitisho vya kuchukuliwa hatua na kuweka kambi kwa kufunga maturubali kuonyesha mshikamano na Wapalestina madhulumu wa Ukanda wa Ghaza.

Vuguvugu hilo lililoanza katika Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York wiki iliyopita, linatoa wito kwa vyuo vikuu kukata uhusiano wa kifedha na Israel na kuachana na makampuni ambayo wanasema yanatoa msukumo na kufanikisha vita vya kinyama na vya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni huko Ghaza.

Wapalestina wapatao 34,262 wameuawa shahidi hadi sasa katika mashambulizi ya jeshi la Israel kwenye eneo hilo lililozingirwa, tokea Oktoba 7 pale wakati wapiganaji wa Hamas waliposhambulia vituo vya Wazayuni kusini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel na kuua Wazayuni 1,139 na kuwachukua mateka makumi ya wengine.

Maandamano hayo yanayoongozwa na wanachuo nchini Marekani yamekuwa ya amani na kwa kiasi kikubwa yanafanyika kwa utulivu na bila ya fujo, lakini yamekabiliwa na hatua kali za ukandamizaji katika vyuo vikuu vingi huku kukitolewa madai kwamba yanaakisi chuki dhidi ya Wayahudi.../

 

Tags