May 05, 2024 04:08 UTC
  • Maelfu ya wakimbizi Afrika Mashariki wapoteza hifadhi kufuatia mafuriko

Maelfu ya wakimbizi katika nchi za Afrika Mashariki wamelazimika kuhama maeneo waliyokuwa wamepata hifadhi kufuatia  mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko yaliyoambatana na maafa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) limetaja wakimbizi walioathiriwa ni wale walioko Tanzania, Kenya, Somalia na Burundi.

Akizungumza na wanahabari mjini Geneva, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Olga Sarrado amesema, shirika hilo lina wasiwasi  kuhusu jinsi maelfu ya wakimbizi na watu wengine waliopoteza makazi wanavyolazimika kukimbia tena kuokoa maisha yao baada ya makazi yao kusombwa na maji.

Nchini Kenya, takribani watu 20,000 katika kambi za wakimbizi za Dadaab wamepoteza makazi yao kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji -wengi wao wakiwa wale waliokimbia Somalia kutokana na ukame.

Katika mji mkuu wa kibiashara wa Burundi, Bujumbura, familia za wakimbizi pamoja na raia wengi, ikiwa ni pamoja na wazee, wamekuwa wakilazimika kuhama mara kadhaa kufuatia viwango vya maji kuendelea kuongezeka.

Tanzania nayo pia imekumbwa na janga hili ambapo zaidi ya wakimbizi 200,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi walioko  katika kambi za wakimbizi za Nyarugusu na Nduta mkoani Kigoma, kaskazini-magharibi mwa Tanzania nao wameathirika. Ofisi ya UNHCR iliyoko  Kigoma nayo imefurika.

Msemaji huyo wa UNHCR amesema kuwa mafuriko haya yanadhihirisha pengo katika maandalizi na hatua za mapema kwani  fedha zilizopo kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hazifiki kwa wale wanaolazimika kukimbia makwao wala jamii zinazowahifadhi. Wakati huo huo, nchi hizi zinakumbwa na ukosefu wa mikakati ya kujiandaa, kuhimili, na kukabili majanga yanayoletwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mafuriko katika nchi za Kenya na Tanzania yamepelekea watu wasiopungua 350 kufariki dunia na idadi hiyo inatazamiwa kuongezeka huku mvua zikilendelea kunyesha.