Apr 29, 2024 07:19 UTC
  • Iran leo inaadhimisha Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi

Wananchi wa Iran leo wanaadhimisha Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi, ambayo ni nembo ya misimamo isiyoyumba ya kukabiliana na njama za baadhi ya nchi za kikanda za kutaka kubadilisha jina la eneo hilo la kistratijia la maji.

Siku ya leo ya tarehe 10 Ordibehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani inafahamika kuwa Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi. Siku hii jina hilo kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuipa majina mengine yasiyo na msingi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson.

 

Kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya utajiri yakiwemo mafuta na gesi, Ghuba ya Uajemi na pwani yake inahesabika kimataifa kuwa sehemu yenye umuhimu mkubwa na ya kistratijia. Kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa la Iran, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliitangaza siku ya leo ambayo inakumbusha tukio la kuwaondoa Wareno kutoka lango la Hormuz, kuwa siku ya taifa ya Ghuba ya Uajemi.

Ghuba ya Uajemi - ambayo ina urefu wa kilomita za mraba 251,000 - inapakana na Mto Arvand upande wa kaskazini, ambao ni mpaka kati ya Iran na Iraqi, na Mlango Bahari wa Hormuz kusini, unaounganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman na Bahari ya Hindi.

Tags