Kuongezeka biashara ya nje ya Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Takwimu zilizochapishwa na Kituo cha Takwimu cha Umoja wa Ulaya (Eurostat) zinaonyesha kuwa mabadilishano ya kibiashara kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wanachama 27 wa umoja huo yaliongezeka kwa asilimia 8 katika robo ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka iliopita.
Mabadilishano kati ya pande hizo mbili katika robo ya kwanza ya mwaka jana yalifikia euro bilioni moja na milioni 180, ambapo yalifikia euro bilioni moja na milioni 276 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Mauzo ya Umoja wa Ulaya kwa Iran mwaka 2023 hadi Machi 2024 mwaka huu yaliongezeka kwa asilimia 10 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita na kufikia euro bilioni moja na milioni 60, lakini katika kipindi hiki uagizaji wa Umoja wa Ulaya kutoka Iran ulipungua kwa asilimia asilimia 3 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa kituo cha takwimu cha Umoja wa Ulaya Ujerumani, Italia na Romania walikuwa washirika wakuu wa kibiashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran barani Ulaya katika robo ya kwanza ya 2024.

Biashara ya Ujerumani na Iran katika robo ya kwanza ya mwaka huu imefikia euro milioni 401 na ukuaji wa asilimia 10, ambapo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana mauzo ya nje ya Ujerumani kwa Iran yameongezeka kwa asilimia 18 hadi euro milioni 343, lakini uagizaji wa nchi hii kutoka Iran umefikia Euro milioni 58 na hivyo kushuka kwa asilimia 23.
Biashara ya Italia na Iran katika robo ya kwanza ya 2024, imeongezeka kwa asilimia 8 hadi euro milioni 189 na biashara ya Romania na Iran imeongezeka mara mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana na kufikia euro milioni 124, wakati uagizaji bidhaa wa nchi hii kutoka Iran haujabadilika na kubakia katika kiwango cha euro milioni 10.
Baada ya Ubelgiji, Ufaransa imekuwa mshirika wa tano wa kibiashara wa Iran katika Umoja wa Ulaya katika robo ya kwanza ya mwaka huu ambapo imebadilishana bidhaa zenye thamani ya euro milioni 77 na Iran, kiwango ambacho kimeongezeka kwa asilimia 7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Takwimu hizi zinapasa kuzingatiwa kwa kutilia maanani masuala kadhaa:
Suala la kwanza ni kuwa ongezeko la biashara kati ya Iran na Umoja wa Ulaya limetimia katika mazingira ya kuongezeka biashara kati ya Iran na Marekani.
Awali, Ofisi ya Takwimu ya Marekani ilitangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Marekani katika miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu yalifikia dola milioni 27.7, ambalo ni ongezeko la asilimia 103 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa ripoti hii, katika miezi mitatu ya kwanza ya 2024, mauzo ya nje ya Marekani kwa Iran yalikua kwa asilimia 77, na uagizaji wa nchi hii kutoka Iran uliongezeka mara 20 katika robo ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, kutoka dola milioni 0.2 hadi dola milioni 3.9.
Pili ni kuwa kuongezeka uhusiano wa kibiashara wa Umoja wa Ulaya na Marekani na Iran kunaashiria uwezekano kuwa pande hizo za Magharibi zimehisi hatari ya kuimarika uhusiano wa Iran na madola mengine hasimu ya Magharibi dhidi yao, na vile vile ombwe lililoachwa nyuma na kujiondoa kwa upande mmoja Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na hivyo kuchukua uamuazi wa kufidia suala hilo.
Uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kundi la BRICS, Jumuiya ya Shanghai Mkataba wa ushirikiano wa miaka 20 na Russia na ushirikiano wa miaka 25 na China ni miongoni mwa mafanikio ya serikali ya Ayatullah Shahid Rais Ebrahim Raisi katika kipindi chake kifupi cha uongozi alichotumikia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Suala la tatu ni kwamba hata kama uhusiano wa kisiasa wa Iran na Umoja wa Ulaya umekumbwa na misukosuko kutokana na ushirikiano wa umoja huo na Marekani katika kutekeleza vikwazo vya kikatili na kidhalimu vya Marekani dhidi ya Tehran, lakini uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande hizi mbili umedumishwa na unaendelea kuimarika.
Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa Iran na Bara Ulaya umekita zaidi katika eneo la Ulaya ya Kati na Mashariki ambalo linajumuisha nchi 14.
Kanda hiyo ina wakazi wapatao milioni 120, pato la taifa la dola bilioni 1200, ukuaji wa wastani wa uchumi wa asilimia 4 na kiwango cha cha biashara yake ya nje kilikuwa karibu dola bilioni 1530.
Pamoja na hayo lakini uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Iran na Umoja wa Ulaya bado uko chini ya kiwango kinachohitajika ambapo kuondolewa vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran kunaweza kutoa fursa nzuri jwa ajili ya kunyanyuliwa kiwango cha sasa cha mabadilishano ya kibiashara ya pande mbili.
Iwapo vikwazo hivyo vitaondolewa bila shaka bara la Ulaya litakuwa miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya mauzo ya nje na uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kama ilivyokuwa huko nyuma kwa sababu kuna uwezo mkubwa wa pande zote mbili kukidhi mahitaji ya soko la kila mmoja.