Bagheri Kani: Iran ina uwezo wa kuchora njia za mafanikio za ulimwengu ujao kupitia BRICS
(last modified Wed, 12 Jun 2024 11:22:55 GMT )
Jun 12, 2024 11:22 UTC
  • Bagheri Kani: Iran ina uwezo wa kuchora njia za mafanikio za ulimwengu ujao kupitia BRICS

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Tehran kwa kuwa kwake mwanachama wa BRICS inaweza kushiriki katika kuchora njia na muongozo mkuu wa ulimwengu ujao kwa kushirikiana na madola mengine.

Ali Bagheri Kani amesema hayo kabla ya kuondoka Nizhny Novgorod, Russia, eneo ulikofanyika mkutano wa BRICS na kutilia mkazo uwezo wa kundi hilo katika kukabiliana na msimamo wa upande mmoja wa madola ya Magharibi hasa Marekani.

Amesema: BRICS inaamini kuwa upande mmoja unaongozwa na Wamarekani si pekee wenye nguvu duniani na kwamba mrengo huo wa Marekani hauwezi kuyapatia suluhisho matatizo ya kimataifa bali ni kinyume chake; muda wote unasababisha matatizo na kuifanya hali ya kimtaifa kuwa ngumu zaidi. 

BRICS mpya na wanachama wapya

 

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia pia hali ya Ukanda wa Ghaza na kusema kuwa huo ni mfano wa wazi wa matatizo yaliyosababishwa na mrengo wa Marekani duniani.

Amesema: Kwa upande mmoja, Marekani inauunga mkono utawala wa Kizayuni kwa silaha kali, angamizi na za kisasa kabisa kwa ajili ya kuua kwa umati watu wa Palestina na kwa upande wa pili inadai kuwa eti ni kiranja wa kutetea haki za binadamu duniani na eti inakuja na mpango wa kutatua mgogoro huo.

Vile vile amesema: Matumaini ya kimataifa yamepatikana hivi sasa kwa kujitokeza na kupata nguvu kundi kama la BRICS ambalo linaonesha kuwa na dhamira ya dhati ya kushirikisha nchi zote kwa usawa katika ngazi ya kimataifa kulingana na uwezo wa kila nchi.