Jun 17, 2024 10:52 UTC
  • Wanaojifanya kutetea haki za binadamu, wanashiriki kwenye mauaji ya watoto Ghaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, wale wanaojigamba kuwa ni viranja wa kutetea haki za binadamu, wanashiriki katika mauaji ya umati dhidi ya watoto wadogo yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.

Nasser Kan'ani amesema hayo leo Jumatatu katika ukurasa wake wa mtandao mmoja wa kijamii na huku akiashiria matamshi ya  James Elder, Msemaji wa Mfukowa Umoja wa mataifa wa Kuwaunga Mkono Watoto aliyekiri kwamba vita vya Ghaza ni vita dhidi ya watoto wadogo na kuandika: Wale wanaojifanya kupigania haki za binadamu wanashirikiana na viongozi wa utawala wa Kizayuni kufanya jinai za kuwaua kidhulma watoto wadogo, jinai ambazo hadi hivi sasa zinafanyika mbele ya macho ya walimwengu na taasisi zenye majigambo mengi za kimataifa vila ya kuchukuliwa hatua zozote za kuwahami, kuwalinda na kuwaokoa watoto hao wa Palestina.

Hayo yamekuja huku kamati ya kutafuta ukweli ya Umoja wa Mataifa ikiwa imetangaza hivi karibuni kuwa, utawala unaokalia kwa mabavu wa Quds tukufu umefanya "maangamizi" ya Wapalestina kwenye vita vinavyoendelea dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Ripoti ya tume hiyo imeeleza kuwa, mauaji dhidi ya Wapalestina, kuteswa kwa misingi ya jinsia dhidi ya wanaume na wavulana wa KPalestina, kulazimishwa kuyahama makazi yao, mateso na ukatili wa kinyama dhidi ya Wapalestina ni miongoni mwa jinai nyingi zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika vita vya Ukanda wa Ghaza.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Ghaza licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mapigano mara moja katika ukanda huo.