UN: Tuna hamu ya kushirikiana na Rais mpya wa Iran
(last modified Tue, 09 Jul 2024 07:54:07 GMT )
Jul 09, 2024 07:54 UTC
  • UN: Tuna hamu ya kushirikiana na Rais mpya wa Iran

Stephane Dujarric Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa taasisi hiyo ya kimataifa ina hamu ya kushirikiana na Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Stephane Dujarric jana Jumatatu alikuwa na mkutano na waandishi wa habari ambao walimuuliza juu ya mtazamo wa Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uchaguzi wa Rais wa Iran ambapo alijibu kwa kusema: "Tuna hamu ya kushirikiana na Rais mpya wa Iran."  

Stephane Dujarric, Msemaji wa UN

Hii ni katika hali ambayo Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imekariri matamshi yake ya kuingilia mambo ya ndani ya Iran kwa kudai kuwa uchaguzi wa karibuni haukuwa huru na wa kiadilifu na kwamba matokeo ya uchaguzi huo hayataathiri pakubwa hatua za Marekani mkabala wa Iran. Matamshi haya ni radiamali ya awali iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kuhusiana na matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais wa Iran. 

Jumamosi iliyopita Msemaji mmoja wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani alitoa radiamali yake ya kwanza kwa matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Iran uliofanyika Ujumaa iliyopita na kudai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru wala wa kiadilifu na kwamba hautaleta mabadiliko ya msingi nchini Iran.  

Akizugumza na vyombo mbalimbali vya habari vya Marekani, Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani alidai kuwa hatimaye Wairani wengi wameamua kutoshiriki kivyovyote katika uchaguzi huo na kwamba serikali ya Marekani haitarajii uchaguzi huo utaleta mabadiliko ya msingi nchini Iran au kupelekea kuheshimiwa pakubwa kile alichotaja kuwa haki za raia. 

Massoud Pezeshkian amechaguliwa kuwa Rais wa tisa wa Iran baada ya kuibuka na ushindi wa kura milioni 16 na 384,403 kati ya zaidi ya kura milioni 30 zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais wa Iran Ijumaa iliyopita. 

Tags