Jul 13, 2024 02:45 UTC
  • Waandamanaji Kenya: Kuvunjwa baraza la mawaziri hakutoshi, tunataka Rais Ruto ajiuzulu

Vijana wanaoandamana nchini Kenya wamesema kuwa, hawajaridhishwa na hatua ya Rais William Ruto ya kuvunja baraza la mawaziri kwani wanachotaka ni kiongozi huyu kujiuzulu.

Baadhi ya vijana nchini Kenya wamesisitiza kwamba, bado hawajaridhishwa na hatua ya Rais William Ruto ya kulivunja baraza lake la mawaziri, huku wengine wakitahadharisha kwamba wataanza tena kufanya maandamano asipojiuzulu kama rais.

Katika hatua ya kutuliza hali ya mambo, siku ya Alkhamisi Rais Ruto aliwafuta kazi mawaziri wake wote akiwemo Mwanasheria Mkuu, isipokuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na waziri kiongozi ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi.

Rais William Ruto amekuwa chini ya mashinikizo kwa majuma kadhaa sasa

Dakta Ruto amesema shughuli za serikali zitaendelea bila kutatizwa, kwa kusimamiwa na Makatibu wa Wizara, huku akiapa kuwa serikali yake imeazimia kupambana kwa nguvu zote na jinamizi la ufisadi. Amesema baraza jipya la mawaziri litatangazwa baada ya kufanya mashauriano ya kina na wadau na wataalamu wa sekta husika.

Tangazo hilo ni katika mfululizo wa hatua alizochukua Dakta Ruto karibuni kujaribu kutuliza joto na ghadhabu za vijana ambao wamekuwa wakiandamana kwa wiki kadhaa sasa wakilalamikia uongozi mbaya wa serikali ya Kenya Kwanza. Wiki iliyopita, Ruto alipendekeza kupunguzwa kwa matumizi ya serikali na kukopa pesa nyingi zaidi ili kujaza nakisi ya bajeti ya takriban dola bilioni 2.7.

Vijana wa Gen-Z walianza kufanya maandamano mwezi uliopita kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ungechangia kuongezwa kwa viwango vya ushuru; lakini yabadilika na kuwa maandamano ya kukosoa utawala mbaya wa Rais Ruto.