Rais Pezeshkian aonya: Matokeo hasi 'mazito' yanaingojea Israel ikijaribu kuishambulia Lebanon
(last modified Tue, 30 Jul 2024 03:17:01 GMT )
Jul 30, 2024 03:17 UTC
  • Rais Pezeshkian aonya: Matokeo hasi 'mazito' yanaingojea Israel ikijaribu kuishambulia Lebanon

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa matokeo hasi 'mazito' utayapata utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa utafanya kosa kubwa la kushambulia kijeshi Lebanon.

Rais mpya wa Iran ametoa onyo hilo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu Jumatatu na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron.
 
Katika mazungumzo hayo, Pezeshkian ameelezea wasiwasi mkubwa alionao juu ya kuongezeka mvutano katika mpaka wa kusini wa Lebanon na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.
 
Mvutano na wasiwasi umetanda kati ya utawala haramu wa Israel na harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah kufuatia shambulizi la siku ya Jumamosi linalodaiwa kuwa la roketi lililoua watu 12 na kuwajeruhi wengine 40 katika mji wa Majdal Shams katika Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Israel.
 
Wakati Israel inailaumu Hizbullah kwamba ndiyo iliyohusika na shambulio hilo, harakati hiyo ya Muqawama imekanusha vikali madai hayo ya uwongo ya utawala wa Kizayuni juu ya suala hili. Kuna hofu kwamba utawala wa Kizayuni unaweza kulitumia dai hilo la uwongo kupanua wigo wa mashambulizi na vita dhidi ya Lebanon.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo kati ya Pezeshkian na Macron, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza utayarifu wa Tehran wa kuendelea na mazungumzo ya kuondolewa vikwazo ndani ya fremu iliyokubaliwa, na akaongeza kuwa matarajio machache iliyonayo Iran kwa upande wa pili wa mazungumzo ni kutekelezwa ahadi zote za pande husika na kusimamishwa mashinikizo na vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran, na kwamba hatua hiyo itaandaa mazingira ya kuendeleza na kupiga hatua mazungumzo hayo.

 
Amekumbusha kuwa : kwa kuzingatia ripoti zaidi ya 15 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Iran imetekeleza ahadi zake zote katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini Wamarekani na bila ya kutekeleza ahadi zao walichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika makubaliano hayo na kuliwekea vikwazo vya kikatili zaidi taifa la Iran.
 

Pezeshkian ameeleza pia utayarifu wa Iran wa kuboresha uhusiano na Ufaransa kwa msingi wa kuheshimiana na kujenga hali ya kuaminiana.

Macron, kwa upande wake, amesema, ana matumaini kwamba Iran itaendeleza uhusiano wake na Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya wakati wa uongozi wa Rais Pezeshkian.../

 

Tags