Iran yakosoa kuvunjwa chama cha al-Wefaq Bahrain
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekosoa vikali hatua ya Bahrain ya kuvunja chama kikuu cha upinzani nchini humo cha al-Wefaq.
Bahram Ghasemi, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema hatua hiyo ya kuvunjwa chama hicho cha Kiislamu haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuzidisha mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi. Amesisitiza kuwa, vitendo vya aina hii vitafungua mlango wa kutumiwa njia zisizo za amani katika kuzitafutia suluhu changamoto mbalimbali nchini humo. Mahakama moja nchini Bahrain hapo jana ilitangaza kukivunja chama cha al-Wefaq, mwezi mmoja baada ya serikali ya Manama kusimamisha shughuli za chama hicho. Aidha mahakama hiyo iliagiza kuzuiliwa fedha na mali zote zinazomilikiwa na chama hicho cha Kiislamu. Hatua hiyo ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa imeendelea kukosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani. Shirika la haki za binadamu la Human Rights First limesema kuwa huo ni mwendelezo wa wimbi jipya la ukandamizaji wa utawala wa Manama wa kutaka kuvifunga mdomo vyama vya upinzani nchini humo. Juni 14 mwaka huu, Wizara ya Sheria ya ukoo wa Aal Khalifa ilitangaza kusimamishwa shughuli zote za chama cha al Wefaq, siku moja baada ya kumkamata Nabeel Rajab, mkuu wa kituo cha haki za binadamu nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa chama hicho cha Kiislamu anazuiliwa na utawala wa Manama tangu mwezi Disemba 2014, kwa tuhuma za kupanga mapinduzi dhidi ya serikali.