Mahakama: Iran itatumia uwezo wake wote kujibu mauaji ya Haniyah
(last modified Wed, 07 Aug 2024 02:28:39 GMT )
Aug 07, 2024 02:28 UTC
  • Mahakama: Iran itatumia uwezo wake wote kujibu mauaji ya Haniyah

Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatumia uwezo wake wote kulipiza kisasi cha mauaji ya Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS), akiwa mjini Tehran.

Asghar Jahangir, Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran alisema hayo jana Jumanne, wiki moja baada ya Haniyah kuuawa kigaidi na Wazayuni hapa Tehran na kueleza kuwa, Marekani inabeba dhima kwa mauaji hayo, kutokana na hatua yake ya kuunga mkono vitendo vya kigaidi vya utawala huo pandikizi.

Kadhalika amekosoa vikali nafasi ya Marekani katika mauaji mengine ya kigaidi ya Fuad Shukr, kamanda mwandamizi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon aliyeuawa na utawala haramu wa Israel huko mjini Beirut.

Amesema, "Haniyah na Shukr waliuawa katika operesheni za kigaidi na kiwoga za utawala bandia wa Israel, ambao uhai wake unategemea mauaji ya kigaidi ya kupangwa, na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wanaodhulumiwa."

Jahangir ameeleza bayana kuwa: Nafasi ya Marekani katika kuunga mkono na kuuendesha utawala huu mbovu haiwezi kupingwa, na inatoa msingi wa kufunguliwa mashitaka ya kisheria na ya jinai kwa serikali [ya Washington] katika taasisi za kimataifa.

Msemaji huyo wa Idara ya Mahama ya Iran amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itatumia uwezo wake wote wa ndani na kimataifa kujibu mauaji ya kikatili na kidhulma ya Haniyah.

 

Tags