Iran yakadhibisha madai ya kutaka kuingilia uchaguzi wa Marekani
Ofisi ya uwakilishi wa kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imepuuzilia mbali madai kuwa Jamhuri ya Kiislamu inakula njama ya kuathiri matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Taarifa ya ofisi hiyo ya kidiplomasia ya Iran imebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu, kinyume na inavyodai Washington, haijashadidisha 'shughuli zake za kimtandao' ili eti kuathiri matokeo ya uchaguzi huo wa Novemba 5 mwaka huu.
Ofisi ya uwakilishi wa kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imeeleza bayana kuwa: Iran haina lengo au mpango wa kufanya shambulio la kimtandao, na wala haiingilii uchaguzi wa Marekani, ambalo ni suala la ndani la nchi hiyo.
Ofisi hiyo ya Iran katika UN imepinga vikali ripoti iliyotolewa jana Ijumaa na shirika la kiteknolojia la Marekani la Microsoft likidai kuwa, Iran inakula njama ya kuiba na kuvujisha baruapepe, kuanzisha mitandao ya habari bandia, na kuanzisha akaunti feki za wanaharakati mashuhuri, kwa shabaha ya kuathiri matokeo ya uchaguzi wa US.
Marekani imekuwa ikiibua madai ya kichekesho na yasiyo na msingi dhidi ya Iran. Julai mwaka huu, Ofisi ya uwakilishi wa kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ilikanusha madai kuwa Tehran inapanga kuathiri matokeo ya uchaguzi wa Marekani kwa maslahi ya mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump.
Aidha mwezi huo huo, na katika kujibu baadhi ya ripoti zisizo na msingi zilizodai kuwa Iran imeshiriki katika jaribio la kumuua Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa tuhuma hizo hazina msingi wowote na kwamba ni za kichochezi.
Hii ni katika hali ambayo, uchunguzi wa maoni uliofanywa na Reuters/Ipsos mwezi Mei mwaka huu unaonesha kuwa, aghalabu ya Wamarekani wana wasiwasi kwamba matokeo ya uchaguzi wa Novemba 5 huenda yakasababisha ghasia zaidi za kisiasa katika nchi hiyo inayodai kuwa imara kiusalama na kidemokrasia.