Pezeshkian: Uungaji mkono wa Magharibi kwa Israel unahatarisha usalama wa kieneo na kiimataifa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Irian amesema kuwa, kiimya cha jamii ya kimataifa mbele ya jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni na ambazo hazijawahi kurekodiwa katika hiistoria, pamoja na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Magharibi kwa utawala huo dhalimu, ni mambo ambayo yanakwenda kinyume na sheia za kimataifa na yanachochea jinai zaidi kama ambavyo pia yanahatarisha usalama wa eneo hili na dunia nzima kwa ujumla.
Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumanne wakati alipozungumza kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Uingereza, Keir Rodney Starmer na kuongeza kuwa, jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ghaza, vitendo vya kigaidi vya Israel, kimya pamoja na uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa jinai hizo, ni mambo ambayo yanahatarisha usalama wa dunia nzima.
Amesema, msimamo wa Jamhuri ya Kisilamu ya Iran ni kupinga vita katika eneo lolote lile duniani kwani inaamini kuwa vita si kwa manufaa ya nchi yoyote ile lakini wakati huo huo Tehran inasisitiza kuwa ni haki yake kumtia adabu adui mchokozi kama ambavyo hiyo ni haki ya kila nchi duniani.
Rais Pezeshkian ameongeza kuwa, Iran inakaribisha juhudi za kustawisha uhusiano wa pande mbili na kuanza tena mazungumzo ya nyuklia akisisitiza kuwa, kufanikiwa makubaliano yoyote yale kunategemea ni kiasi gani pande husika zitaheshimu maafikiano yaliyofikiwa baina yao.
Kwa upande wake, Keir Starmer, waziri mkuu wa Uingereza amesisitiza kwamba nchi yake inataka vita vya Ghaza vikomeshwe na lianze haraka zoezi la kufikishiwa misaada wananchi wa Ghaza na inaamini kuwa Iran inaweza kusaidia sana katika suala hilo.
Waziri Mkuu wa Uingereza vile viile amesema kuwa, nchi yake ina hamu ya kustawisha zaidi na zaidi uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ina matumaini kwamba Tehran na London zitabadilisha mabalozi haraka iwezekanavyo.