Kipaumbele cha sera za kigeni za Iran; nchi jirani, eneo na muqawama
(last modified Sun, 25 Aug 2024 12:15:56 GMT )
Aug 25, 2024 12:15 UTC
  • Kipaumbele cha sera za kigeni za Iran; nchi jirani, eneo na muqawama

Waziri mpya wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema kuwa kipaumbele cha kwanza katika sera za kigeni ni nchi jirani na kipaumbele cha pili ni kupanua uhusiano na Afrika, Amerika ya Latini na Asia Mashariki.

Ameongeza kuwa kipaumbele cha tatu ni nchi zilizosimama upande wa Iran katika hali ngumu.

Araghchi ameyasema hayo katika mahojiano ya televisheni, siku mbili baada ya kuidhinishwa na bunge kama waziri mpya wa mambo ya nje wa Iran. Araghchi amesisitiza kuwa, "Serikali mpya ya Masoud Pezeshkian itaendelea na sera ya ujirani mwema na kuimarisha uhusiano na nchi za eneo, nchi rafiki na uungaji mkono kwa makundi ya muqawama dhidi ya Uzayuni ya serikali ya awamu ya 13 iliyokuwa ikiongozwa na hayati Sayyid Ebrahim Raisi."

Mkuu huyo mpya wa chombo cha kidiplomasia cha Iran ameashiria pia kupanda na kushuka mara kwa mara kwa uhusiano wa Iran na nchi za Ulaya ambao umeathiriwa na siasa za uadui za Marekani dhidi ya wananchi wa Iran katika miongo miwili iliyopita na kusema kuwa, nchi hizo zimechukua sera na mkondo potovu na wakati mwingine wa kiuadui. Araghchi amesema bayana kwamba, kama mwenendo wa madola hayo utabadilika basi zitakuwa katika kipaumbele cha sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu.

Daktari Masoud Pezeshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Araghchi alikuwa akimaanisha kuifuata Marekani kwa upofu kunakofanywa na nchi za Ulaya, ambapo baada ya kujitoa Washington katika mapatano ya nyuklia (JCPOA) na Iran, ilishadidisha mashinikizo dhidi ya Tehran kwa kuzidisha vikwazo dhidi ya Iran. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nyakati tofauti imekaribisha kwa mikono miwili suala la kuendelezwa uhusiano na Umoja wa Ulaya na pia na nchi za Ulaya, lakini Ulaya haijaonyesha nia yake njema katika kuendeleza uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hali nyingi, na suala hili kwa hakika daima limekuwa likidhuru mahusiano baina ya pande mbili.

Kilele cha suala hili kilikuwa baada ya mwaka 2018 ambapo Donald Trump Rais wa wakati huo wa Marekani aliiondoa nchi yake kinyume cha sheria na kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 yanayojulikana kama JCPOA, na Umoja wa Ulaya haukuchukua hatua yoyote ile ili kulinda maslahi ya Iran kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA.

Ni kwa sababu hiyo, ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni hususan serikali ya 13 imetanguliza mbele siasa za kuondoa mizozo na mivutano katika uhusiano na majirani zake na kuimarisha uhusiano na nchi marafiki za eneo na maeneo mengine ya dunia, na serikali mpya ya awamu ya 14 chini ya uongozi wa Daktari Masoud Pezeshkian imesisitiza mara kwa mara kuendeleza sera hii. Bila shaka, kuishi pamoja na kwa amani na kuimarishwa uhusiano na nchi jirani na za eneo daima imekuwa moja ya misingi ya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini sera hii katika serikali ya awamu ya 13 ya hayati Ibrahim Raisi iliyodumu kwa miaka mitatu ilidhihirika zaidi na ilikuwa na mafanikio mengi. Mfano wa wazi ni kurejeshwa kwa uhusiano na Saudi Arabia na Iran uuliokuwa umevunjika kwa miaka kadhaa.

 

Kuhusiana na suala hilo, Rais wa serikali ya awamu ya 14, Masoud Pezeshkian ambaye amechukua hatamu za uongozi, katika wiki za hivi karibuni, amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba, mtazamo wa sera za kigeni wa serikali yake, sawa na serikali ya 13, ni kudhamini maslahi ya taifa katika medani za kieneo na kimataifa, kwa kuzingatia suala la kuimarisha uhusiano na nchi jirani, za eneo na Waislamu, na vile vile kuunga mkono kadhia ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina na mhimili wa muqawama.

Kwa msingi huo na kwa mujibu wa matamshi ya viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa siasa za nje, Iran inajaribu kuweka uwiano na mlingano katika mahusiano na nchi zote kwa upande mmoja na kwa upande mwingine inajaribu kupanua uhusiano na nchi jirani na nje ya kanda ili kujidhaminia maslahi ya kiuchumi.

Tags