Russia yawafukuza nchini wanadiplomasia sita wa Uingereza kwa ujasusi
Russia imewafukuza nchini humo wanadiplomasia sita wa Uingereza kwa kufanya ujasusi. Russia imechukua hatua hiyo ili kulipiza kisasi kwa vikwazo vipya vya Marekani na Uingereza dhidi yake.
Siku mbili baada ya ziara ya pamoja ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na Uingereza huko Ukraine iliyofuatiwa na kutangazwa vikwazo vipya dhidi ya viongozi kadhaa wa Moscow, ikulu ya Russia (Kremlin) imechapisha nyaraka zenye majina na picha za wanadiplomasia hao sita wa Uingereza ikiwatuhumu kwa kutekeleza hatua zilizo nje ya kanunu za kidiplomasia na kwamba walikuwa wakifanya ujasusi na kuamuru wafukuzwe nchini mara moja.
Kremlin imesisitiza kuwa iwapo wanadiplomasia wengine wa Uingereza watabainika kujihusisha na harakati kama hizo hati zao za kazi na utambulisho zitafutiliwa mbali na kufukuzwa Russia.
Uingereza ni kati ya nchi za Ulaya zilizoipatia Ukraine misaada mingi ya fedha na silaha; na siku tatu zilizopita nchi hiyo pamoja na Marekani, Ujerumani na Ufaransa zimeiwekea Russia vikwazo zaidi ya ishirini.
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema katika radiamali yake kwa hatua ya juzi ya Marekani na Uingereza ya kutuma makombora ya masafa marefu huko Ukraine kwamba: 'Tutafanya maamuzi sahihi kulingana na vitisho ambavyo vitaibuliwa dhidi yetu; na NATO itakuwa imeingia rasmi katika medani ya vita na Russia ikiwa itairuhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu dhidi yetu.'