Kiongozi Muadhamu: Kuna udharura wa kulinda utambulisho wa Umma wa Kiislamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kulinda utambulisho wenye thamani wa Umma wa Kiislamu ni dharura na kuongeza kuwa: "Kadhia ya 'Umma wa Kiislamu" haipaswi kusahaulika hata kidongo.
Kwa mujibu wa Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumatatu alipokutana na Maulamaa, Maimamu wa Swala ya Ijumaa pamoja na wakurugenzi wa Madrassah za Ahul Sunna kutoka kote Iran kwa munasaba wa kuanza Wiki ya Umoja wa Kiislamu sambamba na siku za kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW).
Katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei amesema kuna udharura wa kulinda utambulisho wenye thamani wa 'Umma wa Kiislamu' na kusisitiza kuhusu umoja wa Kiislamu. Huku akiashiria njama za wasiowatakia mema Waislamu ambao wanavuruga umoja huo amesema: "Kadhia ya Umma wa Kiislamu haipaswi kusahauliwa."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "Suala la utambulisho wa Umma wa Kiislamu ni suala la kimsingi ambalo linavuka utaifa na mikapa ya kijiografia." Amesisitiza kuwa uhakika na utambulisho wa umma wa Kiislamu haubadiliki."
Ayatullah Khamenei ameashiria njama za mahasimu za kuwafanya Waislamu wapuuze au wasijali kuhusu utambulisho wao wa Kiislamu na kuongeza kuwa: "Ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu wakati Mwislamu anapoghafilika kuhusu masaibu ya Waislamu wenzake huko Gaza na maeneo mengine duniani."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito kwa Maulamaa wa Ahul Sunna, kufungamana na utambulisho wa Kiislamu na umma wa Kiislamu ambapo ameashiria pia mipango na harakati zenye historia ndefu za wasiowatakia mema Waislamu ambao wamekuwa wakiibua migonganao ya kimadhehebu katika Ulimwengu wa Kiislamu na hasa nchini Iran na kusema: "Wanatumia mbinu za kiakili, kifikra, kipropaganda na kiuchumi ili kuwatenganisha Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni nchini na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu." Ametaja moja ya mbinu zinazotumiwa kuwagonganisha Waislamu kuwa ni kuwafanya wafuasi wa pande mbili kuhasimiana na kubishana ili hitilafu ziendelee kuwepo.
Ayatullah Khamenei amesema njia ya kukabiliana na njama hizi za maadui ni umoja na kuongeza kuwa: "Kadhia ya umoja si mbinu bali ni msingi wa Qur'ani."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema umma wa Kiislamu hauwezi kufikia lengo la kupata nguvu na hishima isipokuwa kwa kuwa na umoja.
Aidha amesema leo moja ya mambo ambayo bila shaka ni wajibu ni kuwaunga mkono wanaodhulumiwa huko Gaza na kote Palestina na iwapo yeyote atakwepa jukumu hili bila shaka Mwenyezi Mungu atamuuliza kuhusu suala hilo.