Araghchi: Iran haijaipa Yemen makombora
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekanusha vikali madai yasiyo na msingi ya Wamagharibi kuwa eti Yemen imepokea makombora kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Masirah ya Yemen jana Jumatatu, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, madai hayo yasiyo na msingi ya nchi za Magharibi ni katika msururu wa tuhuma nyingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa, kuituhumu Iran kuwa inatuma silaha Yemen ni dharau kwa wananchi wa Yemen kwa sababu nchi hiyo ina teknolojia na uwezo wa kuimarisha silaha zake za kijeshi.
Sayyid Araghchi amebainisha kuwa, Yemen imekuwa moja ya pande muhimu katika mhimili wa Muqawama na ina nafasi ya kipekee katika kuunga mkono Gaza.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha kuwa, Yemen ina azma thabiti ya kufanya maamuzi yake yenyewe, na inatumia silaha zake inapopenda.
Jeshi la Yemen limeendelea kuimarisha mifumo yake ya makombora na ndege zisizo na rubani siku baada ya siku.
Jumapili alfajiri na ikiwa ni katika kuendelea kuwatetea wananchi wa Ukanda wa Gaza dhidi ya mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni, Harakati ya Ansarullah ya Yemeni ililenga mji wa Tel Aviv kwa kombora la balistiki ambapo mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel ilishindwa kuzuia kombora hilo.