Iran yazitaka nchi za Kiislamu kuungana kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni
(last modified Sun, 29 Sep 2024 06:09:38 GMT )
Sep 29, 2024 06:09 UTC
  • Iran yazitaka nchi za Kiislamu kuungana kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa nchi za Kiislamu zina wajibu wa kuungana na kushikamana katika kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina na Lebanon.

Ijumaa usiku (Septemba 27, 2024), ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zilishambulia eneo la makazi ya watu kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon na kumuua shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah.

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo na Hussein Ibrahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC pambizoni mwa kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani na sambamba na kuashiria jinai ya Israel ya kumuua kidhulma na kikatili Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kuongeza kuwa, ni jukumu la nchi za Kiislamu kushikamana na kuwa kitu kimoja kupambana na jinai za utawala wa Kizayuni kama ambavyo pia ametoa mwito wa kuitishwa kikao cha dharura cha OIC kwa ajili ya kujadili suala hilo.

Shahid Sayyid Hassan Nasrullah

 

Sayyid Araghchi ameongeza kuwa, hii si mara ya kwanza kwa kambi ya Muqawama kupoteza kiongozi wake muhimu sana na nina yakini kwamba kambi hiyo itaendelea kuwa imara na madhubuti zaidi. Pia ameulaumu Umoja wa Mataifa kwa kutoonesha nia yoyote ya kukomesha jinai za Wazayuni.

Kwa upande wake, Hussein Ibrahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC amelaani jinai za Wazayuni na kuahidi kufanya mazungumzo na nchi wanachama wa OIC kuhusu kuitishwa kikao hicho cha dharura.

Tags