Rais Pezeshkian: Hiki ni kiduchu tu cha uwezo wetu, Netanyahu usicheze na Iran
-
Daktari Masoud Pezeshkian
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Daktari Masoud Pezeshkian amesema "Jibu madhubuti limetolewa kwa uchokozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba jibu hilo ni sehemu ndogo sana ya uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ni baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kutwanga vituo vitatu vya kijeshi karibu na Tel Aviv usiku wa kuamkia leo katika hujuma ya kulipiza kisasi iliyopewa jina la Operesheni True Promise II.
"Kwa mujibu wa haki halali, na kwa lengo la kuhakikisha amani na usalama kwa Iran na eneo la Magharibi mwa Asia, jibu la uhakika limetolewa kwa uchokozi wa utawala wa Kizayuni," amesema Rais Pezeshkian katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Rais Masoud Pezeshkian amongeza kuwa: Operesheni hii imefanywa kwa ajili ya kutetea maslahi ya Iran na raia. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anapaswa kujua kwamba, Iran haitaki vita, lakini itasimama kidete dhidi ya tishio lolote. Hii ni sehemu ndogo tu ya nguvu zetu. Usijihusishe na migogoro na Iran."

"Katika Operesheni Ahadi ya Kweli -2, vituo kadhaa vya anga na rada, pamoja na vituo vya njama na mipango ya mauaji dhidi ya viongozi wa Muqawama na makamanda wa IRGC vimelengwa", imesema taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
IRGC imesema kuwa ingawa maeneo yaliyopigwa yamelindwa na mifumo ya hali ya juu ya ulinzi, lakini 90% ya makombora ya balestiki ya Iran yamepiga kwa mafanikio shabaha zilizokuisudiwa.
"Utawala wa Kizayuni umepatwa na wahka kutokana na uwezo wa kiintelijensia wa kioperesheni wa Jamhuri ya Kiislamu," imeongeza taarifa ya IRGC.