Iran: Tutatoa jibu madhubuti kwa nchi zitakazokubali kutumiwa kutushambulia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i117444-iran_tutatoa_jibu_madhubuti_kwa_nchi_zitakazokubali_kutumiwa_kutushambulia
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Jamhuri ya Kiislamu itajibu mapigo dhidi ya nchi ambazo zitaruhusu anga na ardhi zao zitumiwe kulishambulia taifa hili.
(last modified 2024-10-12T23:14:01+00:00 )
Oct 12, 2024 23:14 UTC
  • Iran: Tutatoa jibu madhubuti kwa nchi zitakazokubali kutumiwa kutushambulia

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Jamhuri ya Kiislamu itajibu mapigo dhidi ya nchi ambazo zitaruhusu anga na ardhi zao zitumiwe kulishambulia taifa hili.

Mohammad Bagher Ghalibaf amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon, akiwa ziarani mjini Beirut jana Jumamosi na kusisitiza kuwa, "Iran ina mahusiano ya amani na nchi zote za Asia Magharibi."

Amesema: Tumeshasisitiza mara kadhaa kwamba, hatutaki kupanuka vita, lakini hakuna shaka tutatoa jibu kali na madhubuti kwa shambulio lolote dhidi ya nchi yetu.

Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imejiweka tayari kikamilifu kulinda mamlaka yake na umoja wa ardhi yake dhidi ya uvamizi na uchokozi wowote kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Spika wa Bunge la Iran ameashiria Operesheni ya Ahadi ya Kweli 2 ambapo Iran iliinyeshea Tel Aviv kwa mvua ya makombora 200 ya balestika Oktoba 1 na kubainisha kuwa, "Katika operesheni hiyo, jibu letu lilikuwa la kijeshi, kwani tulilenga tu vituo vya kijeshi, kijasusi na kiusalama vya Israel." 

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), aliondoka Beirut na kuelekea Geneva, Uswisi jioni ya jana Jumamosi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Lebanon.