Araqchi akanusha Iran kuipatia Russia makombora ya balistiki
Iran kwa mara nyingine tena imekadhibisha madai kuhusu kuipatia Russia makombora ya balistiki kufuatia ripoti kwamba Umoja wa Ulaya utatumia tuhuma hizo kama kisingizio cha kuwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu.
Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza haya leo katika ujumbe aliotuma katika ukurasa wake wa mtandao wa X siku mbili baada ya shirika la habari la Reuters kuripoti kuwa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wataidhinisha vikwazo kwa shakhsia na taasisi 14 yakiwemo mashirika ya ndege na kampuni nyingine wakidaiwa kusafirisha makombora ya Iran nchini Russia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hivi na hapa ninamnukuu: "Nilisha tamka wazi, na kurudia tena: Hatujawahi kuipatia Russia makombora ya balistiki."
Abbas Araqchi pia amebainisha kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Iran na Russia si mpya na akasema uhusiano huo una historia ndefu inayorejea miaka kadhaa nyuma kabla hata ya kuanza mgogoro wa Ukraine.
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kuwa nchi za Ulaya ambazo zimeupa utawala wa Israel "silaha za kisasa, na kushiriki kwa wasiwasi katika operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran, sasa zinajaribu kuifurahisha Israel kwa kuibua tuhuma dhidi ya Tehran ili kutekeleza vikwazo dhidi ya Iran.
Mwezi uliopita Marekani ililiwekea vikwazo vipya shirika la ndege la Iran (Iran Air) ambapo Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani pia zilitangaza kutekeleza hatua sawa na hiyo kuhusu kile kilichodaiwa na nchi hizo kuwa IRan inapeleka Russia makombora ya balistiki.