Imam Khamenei: Hizbullah iko hai na inastawi
(last modified Fri, 25 Oct 2024 03:29:27 GMT )
Oct 25, 2024 03:29 UTC
  • Imam Khamenei: Hizbullah iko hai na inastawi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amempongeza Sayyed Hashem Safieddine, kiongozi wa ngazi za juu wa Hizbullah aliyeuawa shahidi hivi karibuni katika hujuma ya utawala haramu wa Israel, na kuitaja harakati ya muqawama kuwa "mtetezi shupavu zaidi wa Lebanon na ngao madhubuti zaidi dhidi ya uroho wa utawala wa Kizayuni." Aidha amesisitiza kuwa, Hizbullah iko hai na inastawi.

Katika ujumbe uliotolewa siku ya Alhamisi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Alikuwa mmoja wa watu mashuhuri wa Hizbullah na sahibu  wa kudumu wa Sayyed Hassan Nasrallah. Ilikuwa ni kwa hekima na ujasiri wa viongozi kama yeye kwamba Hizbullah iliweza kuilinda Lebanon kutokana na tishio la kusambaratika, na kufanikiwa kuondoa tishio la utawala ghasibu, ambao wakati fulani jeshi lake katili lilifika hadi Beirut."

Aidha amesema: "Ujasiri na kujitolea muhanga yeye na makamanda wengine na wapiganaji wa mhimili wa Nasrallah zilikuwa nukta muhimu katika kuondoa tishio la utawala wa Kizayuni kukalia kwa mabavu na kunyakua maeneo ya kusini mwa Litani, Tyre na miji mingine ya eneo hilo."

Kiongozi Muadhamu amesema: "Juhudi zao ziliilinda Lebanon dhidi ya kumezwa ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hizbullah ilitoa muhanga maisha ya wapiganaji wake, rasilimali na itibari yake ili kulinda ardhi ya Lebanon, na kwa njia hiyo kusambaratisha uroho wa utawala wa kichokozi wa Kizayuni."

Akiwahutubu wale wote wanaojali yanayojiri Lebanon, Kiongozi Muadhamu alisisitiza umuhimu wa "jukumu la kujitolea la Hizbullah," na kuutaka umma kutoruhusu madai ya uongo ya adui kuhusu Hizbullah kurudiwa.

Kiongozi Muadhamu amesema: "Leo Hizbullah inasalia kuwa mlinzi hodari wa Lebanon na ngao imara zaidi dhidi ya uroho wa utawala wa Kizayuni, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukilenga  kuibua mgawanyiko nchini Lebanon. Adui anataka kuipokonya Hizbullah jukumu la kulinda Lebanon. Wale wanaoijali Lebanon wasiruhusu kukaririwa madai ya uongo ya adui."

Ayatullah Khamenei pia amesisitiza kuwa Hizbullah iko hai na inastawi, na kuongeza kuwa, "Kama kawaida, Jamhuri ya Kiislamu, kwa irada ya Mwenyezi Mungu, itawaunga mkono wapiganaji wa Al-Quds na wale genge la wahalifu wakaliaji mabavu ambao wameiteka ardhi ya Palestina."

Kiongozi pia alitoa pongezi na rambirambi kwa familia, wapiganaji wenza, na harakati ya Hizbullah kufuatia kuuawa shahidi Sayyid Safieddine.