Rais wa Iran: Njama za Marekani zitasambaratishwa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Utekelezaji wa yaliyoafikiwa katika mkutano wa BRICS utasambaratisha njama za Marekani na washirika wake.
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo usiku wa kuamkia Ijumaa aliporejea Tehran kutoka mkutano wa wakuu wa nchi za BRICS huko nchini Russia. Ameongeza kuwa: "BRICS inakusudia kukabiliana na sera za Marekani na maamuzi ya upande mmoja ya Marekani hasa kuhusu sarafu ya dola." Amebaini kuwa: Katika mkutano wa BRICS, iliamuliwa kuundwa mfuko mpya wa kukabiliana na ukiritimba wa Marekani ndani ya Mfuko wa Kimataifa wa Fedha. Amesema BRICS inalenga kusambaratisha vikwazo vya Marekani na kuwezesha nchi wanachama kuwa na mabadilishano ya kifedha kwa njia salama.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kushiriki rasmi katika kikao cha BRICS kama mwanachama rasmi.
Kufuatia mwaliko wa Rais Vladimir Putin wa Russia Rais wa Iran alielekea Russia Jumanne kushiriki katika mkutano wa 16 wa viongozi wa BRICS uliofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 24 za mwezi huu wa Oktoba.
Kundi la nchi zinazoibukia kiuchumi zinazojulikana kwa jina la BRICS lilianzishwa mwaka 2006 na Brazil, China, India na Russia; na kisha Afrika Kusini. Mwaka huu Iran, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Ethiopia zilijiunga rasmi na BRICS.