Iran yasema vitendo ni muhimu kuliko matokeo ya uchaguzi Marekani
(last modified Mon, 11 Nov 2024 13:30:10 GMT )
Nov 11, 2024 13:30 UTC
  • Iran yasema vitendo ni muhimu kuliko matokeo ya uchaguzi Marekani

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema utendaji wa Marekani kuhusu masuala ya kieneo na jinai za utawala wa Israel huko Gaza na Lebanon pamoja na sera zake kuhusu Iran ni muhimu zaidi kuliko matokeo ya uchaguzi wa nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari wa kila wiki siku ya Jumatatu kwamba Marekani imeendeleza siasa zake za chuki dhidi ya Iran katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Amesema: "Sote tunajua kwamba sababu kuu za kuendelea na kupanuka jinai za utawala wa Kizayuni ni uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huu, kutuma silaha na kuzuia kupitishwa azimio lolote dhidi ya utawala huu katika majukwaa ya kimataifa."

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameelezea matumaini yake kuwa utawala mpya wa Marekani utazuia kuongezeka kwa vita na kwamba viongozi wa Marekani wajifunze kutokana na hali inayoendelea katika eneo na kushikamana na ahadi zao.

Akijibu swali kuhusu madai ya kuhusika kwa Iran katika njama ya kuwaua maafisa wa zamani na wa sasa wa Marekani, akiwemo Rais Mteule Donald Trump, Baghaei amesema inasikitisha kwamba maafisa wa Marekani wanatumia muda na nguvu zao kutoa madai ambayo hayana msingi wowote.

Kuhusu jinai za utawala wa Israel, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema utawala wa Israel umekuwa ukitumia sayansi na teknolojia katika miaka ya hivi karibuni kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.