Araghchi: Iran itatoa majibu kwa Israel katika wakati itakaoona unafaa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia jinai ya Israel ya kushambulia ardhi ya Iran na kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu itatoa majibu kwa utawala wa Kizayuni katika muda inaoona unafaa na kwamba Tehran bado inahifadhi haki yake ya kutoa majibu makali kwa Israel.
Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo mbele ya makamanda na wafanyakazi wa Komandi Kuu ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kuongeza kuwa, Iran imeitangazia rasmi jamii ya kimataifa kwamba shambulio la Israel dhidi ya Iran ni shambulio la kichokozi, linapaswa kujibiwa na Jamhuri ya Kiislamu itatoa majibu hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu imekuwa makini sana na imetumia busara kubwa katika maamuzi yake na kwamba katika majibu ya Ahadi ya Kweli 3 pia, itafanya hivyo hivyo.
Vile vile amesisitiza kuwa, medani ya diplomasia na medani ya mapambano ya moja kwa moja ya silaha zote ziko kwenye kambi moja na zimeshikamana vilivyo.
Ameongeza kuwa, nguvu za kidiplomasia zinatokana na nguvu za kivitendo na za kwenye medani ya moja kwa moja ya mapambano na kwamba kama nguvu za kiulinzi zitakuwa dhaifu, nguvu za kidiplomasia nazo zitakuwa dhaifu.