Iran yakaribisha kusitishwa vita Lebanon, yasisitiza kuwaunga mkono wananchi na Hizbullah
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119418-iran_yakaribisha_kusitishwa_vita_lebanon_yasisitiza_kuwaunga_mkono_wananchi_na_hizbullah
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekaribisha makubaliano ya usitishaji vita kati ya Hizbullah na Israel, na kusisitizia uungaji mkono thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu kwa serikali ya Lebanon, wananchi na harakati yake ya Muqawama.
(last modified 2025-10-22T06:10:45+00:00 )
Nov 27, 2024 12:42 UTC
  • Iran yakaribisha kusitishwa vita Lebanon, yasisitiza kuwaunga mkono wananchi na Hizbullah

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekaribisha makubaliano ya usitishaji vita kati ya Hizbullah na Israel, na kusisitizia uungaji mkono thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu kwa serikali ya Lebanon, wananchi na harakati yake ya Muqawama.

Esmaeil Baghaei, ameeleza katika taarifa aliyotoa leo Jumatano, ambapo sambamba na kutilia mkazo uungaji mkono thabiti wa Iran kwa serikali, wananchi na Muqawamai wa Lebanon amesema,Tehran kwa muda mrefu imekuwa ikisisitiza haja ya kusitishwa mara moja uvamizi wa Israel dhidi ya Ghaza na Lebanon, na imefanya juhudi kubwa za kidiplomasia kwa kipindi cha miezi 14 sasa ili kufikia lengo hilo.
 
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, sera za uvamizi na ushupaliaji vita za utawala wa Kizayuni, ukiungwa mkono kikamilifu na Marekani na baadhi ya mataifa ya Ulaya, zimepelekea wananchi madhulumu na wasio na hatia 60,000 wa Palestina na Lebanon kuuawa shahidi, kujeruhiwa 120,000, na kuwafanya wengine zaidi ya milioni 3.5 walazimike kuyahama makazi yao, mbali na uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu uliofanywa katika Ukanda wa Ghaza na Lebanon.
Esmael Baghaei

Katika taarifa yake hiyo, Baghaei amesema: "kwa kuzingatia maamuzi ya muda ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) yaliyoagiza kuzuiwa vitendo vya mauaji ya kimbari [huko Ghaza], na maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya kutoa hati ya kuwakamata viongozi wa utawala wa Kizayuni kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, maoni ya umma duniani yamekuwa yakitaka kukomeshwa vita na mauaji ya kimbari kwa muda wote wa miezi 14 iliyopita; hivyo sasa yanatarajia kuona wahalifu wa utawala ghasibu wanafunguliwa mashtaka na kuadhibiwa".

 
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kulinda amani na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia, na kutoa mashinikizo athirifu kwa utawala ghasibu wa Israel ili usimamishe vita dhidi ya Ghaza.
 
Usitishaji vita kati ya Israel na Hizbullah ulianza saa kumi alfajiri ya leo kwa saa za Lebanon huku kukiwa na matumaini kwamba mapatano hayo yatamaliza kabisa mashambulizi ya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya miji na vitongoji vya Lebanon na kusitisha mapigano ya zaidi ya mwaka mmoja kati ya kusini mwa Lebanon na kaskazini ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel.../