Rais Pezeshkian: Kambi ya Muqawama itashinda njama za magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119640-rais_pezeshkian_kambi_ya_muqawama_itashinda_njama_za_magaidi
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kuboresha ushirikiano na Syria ili kuondokana na mgogoro unaoendelea katika nchi hiyo ya Kiarabu baada ya magenge ya kigaidi kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi yao ya kikatili.
(last modified 2024-12-02T23:21:42+00:00 )
Dec 02, 2024 23:21 UTC
  • Rais Pezeshkian: Kambi ya Muqawama itashinda njama za magaidi

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kuboresha ushirikiano na Syria ili kuondokana na mgogoro unaoendelea katika nchi hiyo ya Kiarabu baada ya magenge ya kigaidi kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi yao ya kikatili.

Rais Pezeshkian amesema hayo kwenye mazungumzo ya simu na Rais Bashar al-Assad wa Syria jana Jumatatu na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuatilia kwa karibu mambo yanayoendelea hivi sasa huko Syria.

Amesema, mashauriano yake na wakuu wa nchi za ukanda huu na hatua za kidiplomasia za Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi vyote hivyo vinalenga kustawisha maelewano na kuwa na uratibu wa pamoja katika vita dhidi ya ugaidi.

Amesema: Bila ya shaka yoyote tutaweza kuzuia njama za Wazayuni za kuvuruga umoja na mshikamano katika safu za Waislamu iwapo tutazidisha ushirikiano na maingiliano mazuri baina ya nchi za Kiislamu.

Sayyid Abbas Araghchi (kushoto) katika mazungumzo na Rais Bashar al Assad wa Syria mjini Damascus

 

Vilevile amesema: "Tunaamini kwamba Syria itashinda tena njama hizi za Wazayuni. Iran inasimama pamoja na serikali ya Syria na watu wake katika mapambano hayo."

Mwaka 2011, Iran ilikuwa nchi ya kwanza kuisaidia Syria baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kukumbwa na wimbi la mashambulizi ya magaidi waliomiminwa nchini humo kutoka kona zote za dunia na kwa kutumia mipaka yote ya Syria.

Kwa mujibu wa Press TV, mwaka wa 2017, vikosi vya Syria, vikisaidiwa na Iran na Russia vilipata ushindi mkubwa dhidi ya genge la ukufurishaji na la kigaidi la Daesh yaani ISIS.

Hata hivyo, baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Syria yaliendelea kuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo na vikosi vamizi vya madola ya kigeni. 

Tarehe 27 mwezi ulioisha wa Novemba, magaidi, wakiongozwa na genge la ukufusiahaji la Jabhatun Nusra walianzisha mashambulizi makubwa zaidi nchini Syria na kudhibiti sehemu za mkoa wa Halab (Aleppo), na kuelekea kusini kwenye mji wa Hama.

Jana Jumatatu, televisheni ya Syria ilitangaza kuwa, takriban magaidi 320 wameangamizwa na vikosi vya serikali karibu na miji ya Halab, Idlib na Hama.